Mlugu atamba kufanya vizuri Olimpiki

DAR ES SALAAM; MWAKILISHI pekee wa Tanzania katika mchezo wa judo anayeshiriki Michezo ya 33 ya Olimpiki, Andrew Mlugu amesema yuko tayari kwa pambano lake la kwanza dhidi ya mpinzani wake kutoka Samoa.

Mlugo atapanda ‘ulingoni’ kesho na kuwa mchezaji wa kwanza kabisa wa Tanzania kuanza mbio za kuwania medali katika michezo ya mwaka huu inayofanyika Paris nchini Ufaransa.

Akizungumza kwa njia ya mtandao kutoka Paris, Mlugu alisema kuwa pamoja na presha kubwa ya ushindi aliyonayo, lakini yuko tayari kwa mchezo huo na ana imani atashinda.

Advertisement

Soma: Serikali yaagiza maandalizi Olimpiki 2028

Alisema kambi ya mwaka mzima aliyoweka Ufaransa chini ya ufadhili wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) imemjenga vizuri kimchezo huo, hivyo ana matumaini atatumia mbinu alizojifunza nchini humo kupata ushindi.

Mlugu alisema yeye atakuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kuingia uwanjani hivyo macho na masikio ya Watanzania wote yatakuwa kwake kuona anaanzaje na ndio maana ana presha ya kutaka kuanza vizuri.

Alisema kuwa anamjua vizuri mpinzani wake, kwani ameshiriki mashindano mengi ya kimataifa, lakini hilo halimzuii ‘kumkalisha’ chini mpinzani wake huyo watakayekutana naye katika pambano la uzito wa kilo 73.

 

View this post on Instagram

 

A post shared by HABARILEO (@habarileo_tz)

Waogeleaji wa timu ya Tanzania, Collins Saliboko na Sophia Latiff wenyewe watashuka katika bwawa la kuogelea Julai 30 na Agosti 3 wakati wakimbiaji wa marathoni, Alphonce Simbu, Gabriel Geay, Magdalena Shauri na Jackline Sakilu watatimua mbio Agosti 10 na 11.

Aidha, Tanzania juzi ilishiriki ufunguzi rasmi wa michezo hiyo yaliyoshirikisha jumla ya wachezaji 10,714 watakaoshiriki katika michezo 32 kuanzia Julai 26 hadi Agosti 11.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi jana alisisitiza kuwa timu ya riadha itatumia vifaa vya Asics na sio vile vya X-teps ambavyo Shirikisho la Riadha (RT) limekuwa likitangaza.