DAR ES SALAAM: SERIKALI imelitaka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuhakikisha vyama vya michezo inaleta mipango yao kwa ajili ya kujiandaa na Michezo ya Olimpiki itakayofanyika mwaka 2028 nchini Marekani.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt Sulemani Serera ameagiza hayo leo katika hafla ya kuaga na kukabidhi bendera ya taifa timu ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya Olimpiki itakayoanza Julai 26 na kumalizika Agosti 11, mwaka huu Paris, Ufaransa.
Amesema lengo ni kuandaa timu na kuhakikisha idadi ya wachezaji inaongezeka ambao wanakidhi viwango vya kwenda kushiriki michuano hiyo mwaka 2028 kwa ajili ya kuipeperusha vema bendera ya Taifa kupitia michezo.
“Mwaka huu tunawakilishwa na wachezaji saba lengo letu ni kuona mwaka 2028 tunapeleka idadi kubwa ya wachezaji na Serikali itaendelea kushirikiana na Mashirikisho ya Michezo ili kufikia malengo yetu,” amesema Dkt Serera.
SOMA: TOC yaanza mikakati ya Olimpiki Paris
Amesema vyama vinahitaji kuweka wachezaji katika mazingira mazuri na kuandaa timu mapema na kuanzia chini, safari hii wanakuwa makini kwenye ngazi ya chini ikiwemo Umiseta na Umitashumta.
“Hatuna shaka juu ya wachezaji kujiandaa vizuri kwenda kushindana watakapokuwa Paris, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu kuwafatilia.”
“Changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na miundo mbinu bado tunapambana nazo kuzitatua, wachezaji wapambanae kufanya vizuri katika michuano hiyo kwa sababu ni sehemu ya maandalizi ya Olimpiki hii ya 2028,” amesema Serera.
Kwa upande wake Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Gulam Abdulla, amesema kupata nafasi ya kushiriki mashindano hayo lazima mchezaji afikie viwango vinavyohitajika na Olimpiki.
“Hatupeleki mchezaji ambaye hajakidhi vigezo vya kushiriki Olimpiki hawa wote wanaokwenda ni wale ambao wamekidhi vigezo,” amessma Gulam.
Katibu Mkuu wa TOC Filbert Bayi amesema maandalizi ya safari hiyo yamekamilika ikiwa pamoja na kupata viza na tiketi kwa ajili ya kusafiria.
Katibu huyo amesema timu hiyo itaondoka kwa makundi ambapo kundi la kwanza litaondoka Julai 22 (mkuu wa msafara), kundi la pili Julai 23 (kuogelea) na kundi la mwisho litaondoka Julai 27( riadha).