MNAZI BAY: Hifadhi bahari tajiri kwa nyangumi, matumbawe

GHUBA ya Mnazi na Maingilio ya Mto Ruvuma ni hifadhi ya bahari iliyoanzishwa Julai 2000 chini ya Sheria Namba 29 ya Hifadhi za Bahari ya Mwaka 1994 ikiwa na eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 650.
Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Dk Redfred Ngowo anasema eneo la kilometa 420 kati ya hizo ni bahari na kilometa 230 ni nchi kavu.
Akizungumza na HabariLEO hivi karibuni, Dk Ngowo anasema hifadhi hiyo imebarikiwa vivutio vingi na vya kipekee ikiwemo viumbe bahari na hifadhi za misitu.
“Mnazi Bay ina vivutio mbalimbali kama matumbawe ambayo bado yako kwenye hali nzuri kabisa hayajaharibika,” anasema.
Anaongeza: “Tuna aina 243 za matumbawe katika eneo letu la hifadhi. Hayo yametunzwa na yako kwenye hali nzuri, hiyo imefanya eneo hili kuwa na aina nyingi za samaki kwa sababu matumbawe ni sehemu nzuri kwa mazalia ya samaki.”
Nyangumi
Dk Ngowo anasema Hifadhi ya Mnazi Bay ni moja ya maeneo yenye nyangumi wengi ambao huonekana hasa kuanzia Julai hadi Novemba.
Anasema katika miezi hiyo, mamlaka ya hifadhi hiyo hufanya Tamasha Maalumu la Nyangumi kila Septemba 10 hadi 15.
“Baadhi ya watu wanadhani nyangumi ni kiumbe ambacho hakipo, lakini ukweli ni kwamba nyangumi yupo na hapa Mnazi Bay wapo wengi sana,” anasema.
Anaongeza: “Awali ilisemekana kwamba hawa nyangumi walikuwa wakipita tu katika eneo hili, lakini tafiti zilizofanyika baadaye zinaonesha kuwa nyangumi wanazaliana na kula katika eneo hili na ndiyo sababu wanakuwa wengi wakati wa msimu.”
Mbali na nyangumi hifadhi hiyo ina zaidi ya aina 10 za samaki aina ya pomboo (Dolphin) wanaovutia watalii kutembelea eneo hilo pia.
Anasema mamlaka za hifadhi hio zimekuwa zikifanya juhudi za uhifadhi kwa kutoa elimu kwa wavuvi kuacha kuwavua nyangumi sambamba na kuongeza doria wakati wa msimu.
Mhifadhi katika hifadhi hiyo, Amos Singo anasema nyangumi wanaotembelea katika hifadhi hiyo kila mwaka kuanzia Julai ni aina ya ‘harpback’.
Anasema ili mtalii aweze kuwaona viumbe hao, analazimika kutembelea majira ya asubuhi kuanzia saa 12, kwa sababu huo ndio muda tulivu.
Faida ya nyangumi katika mazingira
Dk Ngowo anasema mbali na kuwa kivutio kwa watalii nyangumi wana faida katika utunzaji wa mazingira kwa kuwa Mungu amewajaalia uwezo wa kuondoa hewa ukaa katika hewa.
“Nyangumi mmoja ana uwezo wa kuondoa hadi tani 33 za hewa ukaa katika kipindi chote cha msimu wanachokuwa katika hifadhi,” anasema.
Fukwe
Dk Ngowo anasema hifadhi hiyo imejaaliwa ufukwe safi wenye mchanga mweupe usio na uchafu wa aina yeyote hali inayoufanya uvutie kutembelea.
Anasema shughuli za utalii wa kuzamia chini ya maji pia zinafanyika na hutoa fursa kwa watalii kujionea viumbe bahari vilivyoko chini ya maji.
Msitu wa mikoko
Huu ni msitu wa mikoko wenye ukubwa wa ekari 800.
Kwa mujibu wa Dk Ngowo, msitu huo huchukuaa nafasi ya pili kwa ukubwa katika misitu ya mikoko iliyoko nchini ukitanguliwa na ule wa Delta ya Mto Rufiji.
Anasema msitu huo ni moja ya vivutio vya kipekee katika hifadhi hiyo wenye mchango mkubwa katika utunzaji wa mazingira hasa kupunguza hewa ukaa.
Vivutio vingine ni nyasi za baharini na milima ya michanga iliyojitengeneza inayomwezesha mtu kuona nyangumi vizuri kutokea juu.
Ndege
Mbali na vivutio vingine, hifadhi hiyo imejaliwa aina nyingi za ndege wanaofanyiwa uhifadhi katika kisiwa kinachotambulika kwa jina la Kisiwa Kidogo.
Dk Ngowo anasema ndege hao wana tabia ya kuhama kwenda nchi za Ulaya na baadaye kurejea kama wafanyavyo nyumbu wa Serengeti kwenda Maasai Mara nchini Kenya na kisha kurejea.
Ndege hao wanaifanya hifadhi hiyo kuingia katika orodha ya maeneo muhimu yenye ndege ulimwenguni wakiwa katika nafasi ya 28 kwenye orodha hiyo.
Kasa
Kasa ni kobe bahari wanaoelezwa kuwa katika hatari ya kutoweka.
Hifadhi bahari ya Mnazi Bay ni moja ya maeneo yaliyobahatika kuwa na idadi kubwa ya viumbe hao kutokana mazingira mazuri yanayowaruhusu kuzaliana kwa wingi.
Dk Ngowo anasema katika kuhakikisha kizazi endelevu cha kasa, wamekuwa wakiweka msisitizo katika uhifadhi kwa kufuatilia mazalia yao na kuanzia kwenye mayai yaliyotangwa hadi kusindikiza vifaranga kwenye maji.
“Hawa kasa wanapotaga mayai na baadaye vifaranga vikitotolewa huwa vinarudi kwenye maji. Kwa hiyo, huwa tunafanya ufatiliaji kuanzia kwenye mayai, tunapoona wametaga kwenye eneo lisilo salama tunayahamisha lakini kama yako kwenye eneo salama tunaangalia kama yamefunikwa na mchanga tunayaondolea,” anasema.
“Wakishatotolewa tunaendelea kuwafatilia ikiwa ni pamoja na kuwasindikiza wanaporudi kwenye maji.”
Shuhuda za watalii
“Jina langu ni Leonard kutoka Ujerumani niko hapa Mnazi Bay, nimekuwa na wakati mzuri zaidi hapa katika mapumziko yangu kwa sababu imekuwa safari ya kuvutia, tumeona nyangumi aina ya ‘harpback’, wamechangamka sana, wanaruka! Tumepata wasaa wa kupiga picha! Ilikuwa nzuri sana na nimefurahia kuwa hapa.”
Mwingine anasema: “Mimi ni Thomas kutoka Holand, tumefika hapa, tumepanda boti kwa ajili ya kuona nyangumi.”
Anaongeza: “Ni jambo zuri sana, tumeona nyangumi akipiga mbizi chini ya boti na mtoto wake, kila kitu kilikuwa safi, tumerejea na kukaa ufukweni, tumekuwa na wakati mzuri sana.”
Fursa
Akizungumzia fursa za kiuchumi na uwekezaji, Dk Ngowo anasema kunahitajika uwekezaji zaidi kuendeleza utalii kwenye eneo hilo hasa ukizingatia kwamba wao kwa sasa asilimia kubwa wanafanya uhifadhi zaidi hivyo ili kuendeleza utalii uwekezaji zaidi unahitajika.
Anasema kama wawekezaji wanaweza kujitokeza kujenga hoteli katika hifadhi hiyo itachagiza utalii na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea.
Anaongeza kuwa viko visiwa vitatu ambavyo ni Namponda, Nembelwa au Mmongo na Kisiwa Kidogo.
Anasema miongoni mwa visiwa hivyo, Kisiwa Kidogo kinatumika kama hifadhi ya ndege na hakihitaji uwekezaji wowote, lakini visiwa viwili vinavyobaki vinahitaji uwekezaji wa utalii.