Mohammed Iqbal atakumbukwa

DAR ES SALAAM: ATAKUMBUKWA, Mohammed Iqbal, aliyekuwa msomi na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, alikuwa miongoni mwa Watanzaia walioshiriki katika mijadala muhimu kuhusu muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Katika harakati hizo, alitoa pendekezo la jina “Tanzania,” ambalo lilitokana na mchanganyiko wa majina ya Tanganyika na Zanzibar, na hatimaye likakubaliwa rasmi na viongozi wa wakati huo, akiwemo Mwalimu Julius Nyerere.

Katika mahojiano na waandishi wa habari miaka kadhaa nyumba  Mohammed aliwahi kutoa ufafanuzi kuhusiana na jinsi alivyobuni jina hilo loa Tanzania.

Alisema kwa muongozo wa Mungu alichukua herufi tatu za kwanza za Tanganyika (TAN) na herifi tatu za Zanzibar (ZAN) na kisha akaongeza (I) kutoka kwa jina lake Iqbal na Imani yake katika Uislamu. Hatimaye akakumbuka uhusiano wake na madhehebu ya Ahmadiyya na akaongeza (A) ili kuheshimu madhehebu hayo, na hivyo TANZANIA ikatokea.

Mohammed Iqbal alizaliwa katika kipindi cha ukoloni Agosti 8, 1944 na alihusika kwa kiasi kikubwa katika mijadala ya utaifa na harakati za ukombozi wa Tanganyika.

Alikuwa mtu mwenye uelewa wa kina kuhusu historia, utambulisho wa kitaifa, na umuhimu wa mshikamano wa bara na visiwa.

Mnamo mwaka 1964, Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuunda taifa jipya. Kulikuwa na mjadala wa jina gani lingeweza kubeba dhana ya umoja wa nchi hizo mbili, na hapo ndipo Mohammed Iqbal alipoleta wazo la “Tanzania”—jina lililopokelewa kwa furaha na hatimaye kuwa rasmi.

Katika maisha yake, Iqbal aliendelea kuwa mchangiaji mkubwa katika mijadala ya maendeleo ya kitaifa na umuhimu wa utambulisho wa Tanzania. Kupitia mchango wake, jina “Tanzania” limebaki kuwa alama ya mshikamano wa Watanzania na kiashiria cha historia ya taifa.

Kwa kifo cha Mohammed Iqbal, taifa limepoteza mtu muhimu aliyetoa mchango mkubwa katika historia yake. Serikali, viongozi wa kisiasa, wasomi, na wananchi kwa ujumla wanaendelea kuomboleza kifo chake huku wakikumbuka mchango wake usiosahaulika.

Urithi wa Iqbal utaendelea kuishi kupitia jina “Tanzania,” ambalo linawakilisha umoja, mshikamano, na utaifa wa Watanzania wote.

Iqbal amefariki akiwa na miaka 80, na chanzo cha kifo chake kimetokana na kuugua kwa takribani miaka 10, na alikuwa chini ya uangalizi wa karibu nyumbani kwake.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button