MOI yaanza upasuaji kurekebisha viungo

KWA mara ya kwanza, Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeanza kutoa huduma za upasuaji wa kibingwa wa kutibu mishipa ya fahamu iliyoathirika kutokana na ajali katika mikono na miguu kwa wagonjwa wanaokabiliwa na changamoto hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dk. Mpoki Ulisubisya amesema hatua hiyo ni mafanikio makubwa kwa taasisi hiyo na sekta ya afya nchini kwa ujumla. “Tumeanza kwa mafanikio kutibu mishipa ya fahamu iliyopo mikononi na miguuni. Huduma hii itawanufaisha wagonjwa wanaoshindwa kuinua vitu au wanaopata changamoto ya kutembea vizuri baada ya kupata ajali,” amesema Dk. Mpoki.

Ameongeza kuwa kwa sasa huduma hiyo inapatikana MOI pekee nchini, baada ya madaktari wa taasisi hiyo kupata mafunzo ya ubobezi na ujuzi maalum wa kufanya upasuaji huo. “Huduma hii imeanza baada ya daktari wetu kukamilisha masomo ya ubobezi na kupata utaalamu wa kutibu na kufanya upasuaji wa mishipa ya fahamu iliyopata majeraha,” ameongeza.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa Bobezi wa Majeraha ya Mkono na Mguu, Dk. Hellen Machagge, amesema kuwa kujeruhiwa kwa mishipa mikubwa ya fahamu husababisha misuli midogo kushindwa kufanya kazi, hali inayoweza kusababisha kupooza kwa mikono au miguu.

“Katika upasuaji huu tunahamisha mishipa ya fahamu kutoka sehemu moja kwenda sehemu iliyoathirika ili kuuwezesha mkono au mguu kuanza kufanya kazi vizuri kama ilivyokuwa kabla ya kujeruhiwa,” amesema Dk. Hellen.

Hatua hiyo ni muendelezo wa MOI kuanzisha huduma za kibingwa na kibobezi ambazo hazikuwapo nchini, na hivyo kupunguza usumbufu pamoja na gharama kubwa za wagonjwa waliolazimika kufuata huduma hizo nje ya nchi. SOMA: MOI yagawa viungo bandia bure

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button