Muhimbili yaboresha ubebaji wagonjwa wasioweza kujihudumia

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na Shirika la ASK-International imehitimisha mafunzo maalum ya ubebaji bora wa wagonjwa wasioweza kujimudu wenyewe, wakiwemo wagonjwa waliopooza, wazee wanaohitaji msaada wa kubebwa, pamoja na waliopata ajali au kuumia vibaya ili kuwaepusha na athari nyingine za kiafya wakati wa matibabu.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma za Ukunga na Uuguzi MNH, Redemptha Matindi, amesema hospitali ilibaini kuwepo kwa pengo kubwa katika eneo la ubebaji na uhamishaji wa wagonjwa.

Amesema  hatua hiyo italeta nafuu si kwa wagonjwa pekee bali pia kwa wauguzi, kwa kuwa watatumia mbinu za kisasa na salama zaidi bila wagonjwa kujiweka katika hatari ya kupata maumivu au majeraha kazini.

“Lengo kuu ni kupunguza matatizo yanayoweza kujitokeza wakati mgonjwa akihudumiwa, ikiwemo maumivu makali, vidonda vinavyotokana na kulala muda mrefu, hivyo wakufunzi walijikita katika kutoa mbinu bora za kumhamisha mgonjwa kutoka kitanda kimoja kwenda kingine, kutoka kwenye kiti mwendo kwenda kitandani au kinyume chake, bila kumletea madhara mgonjwa wala mhudumu wa afya,” amesema.

Aidha wauguzi kutoka wodi mbalimbali Muhimbili, ndugu wa wagonjwa wanaohitaji msaada wakiwa nyumbani, pamoja na wanafunzi wa uuguzi kutoka Chuo Kikuu cha Kairuki wamenufaika na mafunzo haya.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button