MSANII mkongwe wa filamu nchini Yvone Cherrie ‘Monalisa’ amezindua msimu mpya wa Usiku wa Tuzo za Wanawake zinazoitwa (Woman in Sports, artist and Cultus, (WISAC) zinazotarajia kufanyika Novemba 29 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, mwandaaji wa tuzo hizo, Monalisa amesema tuzo hizo zitakuwa za tofauti na kwamba ni nafasi ya wanawake kuonekana kwa kile wanachofanya.
“Nimeandaa tuzo za wanawake vinara kwenye sekta ya sanaa, michezo na habari, ili kuwapa chachu wanawake kufanya vizuri zaidi ya wanavyofanya,” amesema.
Amesema kuwa tuzo hizo zitatolewa kwa mwanamke bora kwenye michezo, habari, washehereshaji na sanaa za mikono, filamu na sekta mbalimbali ikiwemo ya uongozi kutakuwa na vipengele 30.
Novemba 12 watu wataanza kupiga kura kwenye mitandao ya kijamii Mwafrikaasilia hadi itakapofika Novemba 21 itakuwa mwisho wa kupiga kula.
“Wanafanya vitu vikubwa lakini hawapati nafasi ya kujulikana katika jamii kutokana na wanachokifanya, unachotakiwa ni kumpendekeza mwanamke unayeona anastahili kupata tuzo kutakuwa na majaji watamchagua kutokana na kazi yake, “amesema Monalisa.