Morogoro wapata huduma za kibingwa bure

MOROGORO; Wananchi Mkoa wa Morogoro wamejitokeza kupata huduma za kibingwa na bobezi bure katika maadhimisho ya miaka 20 ya Chuo Kikuu cha Waislam (MUM).
Huduma hizo zinatolewa na Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), ambapo madaktari bingwa na wabobezi wanatoa huduma ya ushauri na matibabu kwa wananchi wa mji wa Morogoro na viunga vyake.
Matibabu hayo yalianza kutolewa Juni 18, 2025 katika viwanja vya chuo hicho na yataendelea kutolewa hadi Juni 20, 2025.
Daktari Bingwa wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya fahamu MOI, Dk Zarina Shabhay amesema ushiriki wa MOI katika maadhimisho hayo umelenga kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.
“Ni fursa adhimu kwao, hivyo hawana budi kuitumia vizuri kwa kujitokeza kwa wingi kupata matibabu haya ya bure…kwetu MOI ni faraja kuwa hapa na kuungana na wanachuo katika maadhimisho haya,” amesema.