Mpango ashiriki kumuombea marehemu askofu Munga

MAKAMU wa Rais Dk Philip Mpango na Mwenza wake Mama Mbonimpaye Mpango wameshiriki Ibada Maalum ya kumuombea aliyekuwa Askofu Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Marehemu Dk Stephen Munga, iliyofanyika Maramba Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga.
Ibada hiyo imeongozwa na Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Askofu Maimbo Mndolwa na kuhudhuriwa na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Askofu Dk Alex Malasusa, Askofu wa Jimbo Katoliki Tanga Mhashamu Thomas Kiangio, Katibu wa Baraza la Waislamu (BAKWATA) Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga Sheikh Muhsin Mohamed pamoja na waumini mbalimbali.
SOMA: Serikali kuendelea kushirikiana na makanisa
Akizungumza na waumini baada ya Ibada hiyo, Makamu wa Rais amesema ushirikiano baina ya Serikali na Taasisi za dini ni muhimu sana kuendelea kudumishwa.
Amewasisitiza viongozi wa dini kuendelea kuliombea Taifa ili liendelee kuwa salama na lenye amani pamoja na kuwaombea viongozi waweze kufanya kazi kwa mapenzi ya Mungu kwa faida ya wananchi.
Aidha Makamu wa Rais amewasihi wananchi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwezi wa Oktoba na kuhakikisha amani inadumishwa wakati na baada ya uchaguzi.
Amesema shughuli zote za kijamii na kiuchumi ikiwemo kufanya ibada zinafanyika vema kutokana na amani iliyopo.
Askofu Mstaafu, marehemu Dk Stephen Munga alifariki dunia Septemba 20, 2025.