Dk Mpango ataka matendo ya Papa yaenziwe

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amesema namna bora ya kumuenzi aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis ni kudumisha amani pamoja na kujali masikini.
Dk Mpango alisema hayo wakati wa mazungumzo baada ya kumalizika kwa misa ya mazishi ya Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, Vatican.
Alisema kiongozi huyo alikuwa mnyenyekevu na mtu aliyefanya jitihada kubwa za utafutaji amani maeneo mbalimbali duniani na kuacha alama, ikiwemo tukio la kuwabusu miguu viongozi wa Sudan ili waachane na mapigano.

Alisema kati ya nyaraka za mwisho alizosaini Papa Francis, ni pamoja na barua aliyomwandikia, Rais Samia Suluhu Hassan kumtakia heri ya Siku njema ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Katika misa hiyo ya mazishi, Dk Mpango aliongozana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania Vatican, Balozi Hassan Mwameta na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme.

Misa ya mazishi ya Papa Francis ilihudhuriwa na zaidi ya watu 250,000 wakiwamo viongozi wakuu wa mataifa mbalimbali duniani. Maziko yalifanyika katika Basilika ya Maria Maggiore jana.



