Mpango kuupandisha hadhi Mji Mdogo Mlandizi waelezwa

DODOMA; HALMASHAURI ya Wilaya ya Kibaha imeelekezwa kufanya michakato iliyoainishwa kwenye sheria na mwongozo wa uanzishwaji wa maeneo ya utawala.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Reuben Kwagilwa, ametoa kauli hiyo bungeni leo Februari 6, 2026, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kibaha Vijijini, Hamoud Abuu Juma, aliyetaka kujua serikali ina mpango gani wa kuupandisha hadhi Mji Mdogo wa Mlandizi kuwa mji kamili.

“Halmashauri huanzishwa au kupandishwa hadhi kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa Sura ya 287 na 288 pamoja na Mwongozo wa uanzishwaji wa Maeneo ya Utawala wa Mwaka 2014, ambao umeainisha vigezo na taratibu zinazopaswa kufuatwa, ili kuanzisha au kupandisha hadhi halmashauri.

“Kwa mujibu wa mwongozo mchakato wa kuanzisha halmashauri mpya huanza na kusudio ambalo hupaswa kujadiliwa katika vikao vya ngazi ya vijiji/mitaa, kata, halmashauri, wilaya na mkoa.

“Kusudio hilo huwasilishwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi kupitia Katibu Tawala Mkoa kwa ajili ya kufanyiwa tathmini na ufuatiliaji ili kuhakikisha ufikiwaji wa vigezo husika.

“Napenda kuielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kufanya michakato, iliyoainishwa kwenye sheria na mwongozo wa uanzishwaji wa maeneo ya utawala,” amesema Naibu Waziri.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button