Mpogolo atoa wito kuutunza muungano

DAR ES SALAAM: KATIKA kusherehekea miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ametoa mwito kwa wananchi kuendelea kuuenzi, kuutunza na kuutetea muungano huo.

Wananchi Wilayani Ilala, Mkoani Dar es salaam, wameungana na Watanzania katika kuadhimisha miaka 61 ya Muungano, huku Mkuu wa wilaya hiyo Edward Mpogolo akitoa wito wa kuendelea kuuenzi, kuutunza na kuutetea Muungano.

Akihutubia wananchi, viongozi na wadau waliojitokeza kufanya usafi wa mazingira leo Aprili 26, 2025 katika soko la samaki Ferry, Mpogolo amesema dhamana ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar  iko kwa kila Mtanzania.

Mpogolo ameeleza kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliotimiza miaka 61 ni kielelezo cha tunu ya Taifa iliyoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Shekh Abeid Amani Karume.

Mpogolo amebainisha katika soko la samaki Ferry, ni sehemu ambayo inadhihirisha Muungano uliopo kwa watanzania wanaofanya biashara katika soko ilo kuwa na muingiliano wa makabila na tabaka tofauti toka upande wa bara na visiwani.

Ameongeza kuwa kauli mbiu ya Miaka 61 ya Muungano, imebeba dhima ya kuchagua viongozi bora kwa kufanyika uchaguzi kila baada ya miaka mitano kwa mujibu wa katiba kumchagua Rais ambaye anajukumu la kuunda serikali na kutunza Tunu hiyo ya Muungano.

Kuhusu suala la Ushiriki wa Uchaguzi Mkuu, Mpogolo amewahimiza wananchi wenye sifa kushiriki zoezi ilo na kuchagua viongozi bora pamoja na kudumisha amani, umoja na mshikamano kwa taifa.

Pia Mpogolo amesema wilaya ya Ilala inaendelea kudumisha umoja, amani na mshikamano kama kielelezo cha Muungano kwa viongozi kuwa wamoja hali inayofanya wilaya hiyo kuwa na amani licha ya kuwa na watu zaidi ya milioni tatu muda wa mchana na zaidi ya watu milioni moja usiku.

Pamoja na kuendelea kupokea wageni kwa njia ya anga, reli na maji wanaofikia Ilala, bado inakuwa na amani jambo linaloendelea kudumisha Muungano kwa kila mmoja kufanya kazi zake bila shurutiwa.

Aidha, Maadhimisho hayo ya Muungano, kwa wilaya ya Ilala yaliyoadhimishwa kwa  kufanya usafi soko la samaki Ferry, upandaji miti katika msitu wa zingiziwa, na usafishaji eneo la fukwe za bahari ya Hindi kwa kushirikiana na Jeshi la Uhamiaji.

Mpogolo, amelipongeza Jeshi ilo kwa ushirikiano na kuendelea kudumisha Muungano na kuhakikisha Ilala inakuwa salama kwa wageni wanaoingia wanafuata sheria za nchi ya Tanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Ilala, Elihuruma Mabelya ametumia nafasi hiyo kuwahimiza vijana kuwa wazalendo na kudumisha Muungano ili uendelee kuwa wa mfano.

Nae, Meya wa Jiji la Dar es salaam, Omary Kumbilamoto amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar licha ya kuwa wa nchi moja  bali umejenga udugu, ujamaa na kuondoa kero zilizokuwa miaka ya nyuma ya kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Jiji la Ilala limeadhimisha Miaka 61 kwa kumpongeza Rais Dokta  Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dokta, Hussein Ally Mwinyi kwa kutunza Tunu ya Muungano na kuleta maendeleo katika sekta zote nchi.

Maadhimisho ambayo yamekwenda na kauli mbiu, ‘Muungano wetu ni Dhamana, Heshima na Tunu ya Taifa, Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025’.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button