MKOA wa Iringa umepata msukumo mpya kupitia Shirika la DSW Tanzania, ambalo kwa kupitia mradi wake wa REST (Reproductive Equity Strategy in Tanzania) litasaidia kuboresha maisha ya vijana kwa kufanya ushawishi na utetezi wa sera na mifumo inayowahusu, ili wapate fursa za kufikia ustawi wa kijamii na kiuchumi.
Mradi huo unaotarajiwa kuleta mabadiliko makubwa, umejikita katika kuchochea mazingira rafiki kwa vijana katika upataji wa huduma za afya ya uzazi, kupunguza ukatili wa kijinsia, kukuza usawa wa kijinsia, na kuliwezesha kundi hilo kujitambua na kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza wakati wa utambulisho wa mradi huo leo mjini Iringa, Mkurugenzi wa DSW Tanzania, Peter Owaga, alisema mradi wa REST utatekelezwa katika kata tisa za mkoa wa Iringa.
Kata hizo ni Kising’a, Kihorogota, Mseke, na Ifunda kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, pamoja na Mtwivila, Kihesa, Makorongoni, Mkwawa, na Ruaha katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.
“Ni mradi wa miaka mitatu, unaoanza mwaka huu 2024 hadi 2027, ambao utasaidia kupunguza changamoto zinazowakabili vijana na wanawake pia huku ukihimiza ushirikiano wa karibu kati ya jamii, serikali, na wadau mbalimbali,” alisema Owaga.
Alisema mradi wa REST umeundwa ili kuhakikisha vijana wanapata fursa za kujifunza stadi za maisha, kupata maarifa ya afya ya uzazi, kupambana na ukatili wa kijinsia na kujitambua ili kufikia fursa za kujikwamua kiuchumi.
“Ni lazima tuwekeze kwa vijana kupitia elimu, afya, fursa za kiuchumi, na maeneo ya kujijenga. Hii ndiyo njia pekee ya kuwawezesha kufanikisha ndoto zao na kuchangia maendeleo ya taifa,” Owaga alisema.
Aliongeza kuwa ushawishi wa sera, utekelezaji wa mipango thabiti na bajeti toshelezi ni msingi wa mafanikio ya mradi huo.
“REST inalenga kuboresha uwezo wa taasisi zinazoshughulika na vijana, kuhakikisha sera zinazowalinda vijana na wanawake na utekelezaji wa mipango yao unakuwa na ufanisi,” alisema.
Kwa mujibu wa Owaga, vijana wanakabiliwa na changamoto nyingi zinazoweza kuathiri maisha yao ikiwa hazitashughulikiwa.
Alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na: Uelewa mdogo wa masuala ya afya ya uzazi. kukosa stadi za maisha na malezi rafiki, ukatili wa kijinsia ikiwemo uongezeka kwa mimba na ndoa za utotoni, maambukizi ya magonjwa ya zinaa, ikiwemo VVU na matumizi ya dawa za kulevya.
Alisema changamoto hizi zikiendelea zinaweza kusababisha athari mbaya kwa maendeleo ya vijana, jamii na taifa kwa ujumla.
“Ni wakati sasa wa kutekeleza kwa vitendo sera ya taifa ya maendeleo ya vijana ya mwaka 2024,” alisisitiza.
Alisema ili kufikia malengo yake, mradi wa REST utatekelezwa kwa kushirikiana na mashirika ya Tahea na Alama Yangu, pamoja na viongozi wa kata husika katika halmashauri hizo kama njia ya haraka ya kuwafikia vijana wa kata hizo.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii ya Manispaa ya Mwantumu Dossi aliihimiza jamii kuwekeza kwa vijana kama kundi muhimu linalotoa daraja la maendeleo ya taifa na akalishukuru shirika ka DSW kwa kuja mkoani Iringa kuwaongezea nguvu.
Akizungumzia changamoto ya ukatili wa kijinsia, Dossi alisema “Takwimu mkoani kwetu zinaonesha zipo juu, ama serikali tunahitaji kushirikiana na wadau kama hawa ili kukomesha vitendo hivyo na kuwasaidia vijana waweze kujitambua, wawe bora na kuchangia uchumi ipasavyo.”