Msajili ataka uvumilivu mchakato Katiba

MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi

MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi ametoa mwito kwa wananchi wawe wavumilivu na waukubali mchakato wa sasa wa mabadiliko ya Katiba ya Tanzania.

Jaji Mutungi amesema uvumilivu huo ni muhimu kujiandaa ili mchakato huo usikwame kama mwaka 2014.

“Mkumbuke kuna mahali imesemekana Mheshimiwa Rais ameshauriwa kilichotokea huko 2014 kukwaza mchakato uliokuwa umeshaanza basi tukwepe kisijitokeze safari hii,” alisema Jaji Mutungi alipozungumza na Kituo cha Televisheni cha Azam cha mkoani Dar es Salaam.

Advertisement

Alisema ni muhimu kutoa muda wa kutoka watu wakae kwenye makundi yanayowahusu ili watoe maoni kupata mawazo ya uwakilishi yatakayopelekwa kwenye kikao maalumu ya Baraza la Vyama vya Siasa.

“Kila mtu alipo kwenye nafasi yake na kwenye kundi lake husika wajiandae na maoni kuntu ambayo wanasema haya tukiwayakilisha yataleta tija katika mchakato mzima wa Katiba,” alisema Jaji Mutungi.

Amesihi wanasiasa na vyama vya siasa waheshimu na kuona umuhimu wa mawazo ya wananchi katika mchakato wa Katiba.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais Samia Suluhu Hassan alimuagiza Jaji Mutungi aitishe kikao maalumu cha Baraza la Vyama vya Siasa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Rais Samia alieleza kuwa lengo la kikao hicho ni kushirikisha wadau kutathmini utekelezaji wa mapendekezo ya kikosikazi kilichoratibu maoni kuhusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini.

Rais Samia alitoa maelekezo hayo wakati wa kikao kilichofanyika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, kilichohudhuriwa na viongozi wa serikali kuhusu kuanza kwa mchakato wa Katiba mpya.

Taarifa hiyo ya Ikulu ilieleza kuwa kikao hicho kilijadili namna ya kushirikisha wadau na hasa ushirikishwaji wa wananchi katika mchakato huo kutoka pande zote mbili Tanzania Bara na Zanzibar.

Alieleza kuwa mbali na mchakato wa Katiba mpya, masuala mengine yanayotarajiwa kushughulikiwa ni marekebisho ya sheria zinazohusiana na uchaguzi zikiwamo Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Sheria ya Vyama vya Siasa.

Hivi karibuni, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro alilieleza Bunge kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024, wizara hiyo imejipanga kutekeleza vipaumbele 30 kikiwamo cha kuratibu mchakato wa Katiba mpya.

Awali Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema katika mwaka wa fedha 2023/24, shughuli za maandalizi ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka 2024 zitaendelea.

Majaliwa alisema hayo bungeni Dodoma wakati akiwasilisha mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/24.