Msako mkali Mwanza kuwabaini wahalifu

Afungwa jela maisha kwa kulawiti hadharani

MWANZA: JESHI Polisi mkoani Mwanza limeendelea kufanya misako mbalimbali dhidi ya watu wanaojihusisha na matukio ya kihalifu ili kuwaepusha wakazi wa mkoa huo na matukio ya uhalifu yanayoweza kusababisha hofu itakayowafanya washindwe kufanya shughuli mbalimbali za kujipatia kipato katika shughuli zao za kila siku sambamba na kuwakosesha amani.

Akizungumza na waandishi wa habari Januari 26, 2024 Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa wakati akitoa taarifa ya kuanzishwa kwa msako maalum kwaajili ya kudhibiti na kuzuia matukio ya kihalifu katika mkoa huo amesema kuwa taarifa kuhusu uhalifu na wahalifu zimeendelea kupatikana kutokana na ukusanyaji wa taarifa fiche zinazohusu wahalifu ambayo ni kazi inayofanywa kwa weledi na askari wa jeshi hilo.

“Taarifa nyingine tumeendelea kuzipata kutoka kwa wananchi wasiopenda uhalifu na kupitia ushirikishwaji mkubwa wa jamii unaofaywa na jeshi la polisi kupitia mikutano kati yetu na wananchi inayoendelea kufanyika katika kata mbalimbali ambapo tumepata mafanikio makubwa katika kuwafichua wahalifu kwenye mitaa mbalimbali”…Alisema Kamanda Mutafungwa

Advertisement

Aidha Kamanda Mutafungwa ameongeza kuwa katika msako wa wiki moja walioufanya wamefanikiwa kuwatia mbaroni washukiwa mbalimbali wa matukio ya kihalifu wakiwemo watuhumiwa wa kujihusisha na vitendo vya uhalifu 47, watano kuingia nchini bila kibali, watuhumiwa wanaojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya 51, watuhumiwa wa mauaji 13 na watuhumiwa wa kuvunja nyumba na kuiba 17.

“Miongoni mwa vielelezo vilivyokamatwa katika msako huo ni simu za aina mbalimbali zaidi ya 50,dawa za kulevya aina ya mirungi,misokoto ya bangi, vifaa vya kufanyia uhalifu pamoja na mali zilizoibiwa sehemu mbalimbali katika makazi ya watu”..Alisema