Mshangama akutana na wazee Kagera, atoa msaada

MJUMBE wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Viti Vitatu Bara, Shamira Mshangama ametembelea kituo cha kulea wazee na wasiojiweza akiwa katika ziara fupi ya kichama Bukoba, mkoani Kagera.

Katika kituo hicho chenye wazee 19 wakiwemo 15 wanaume na 4 wanawake, Shamira alipata muda wa kuzungumza na kuwafikishia salamu kutoka kwa Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohammed Ali Kawaida.

Advertisement

“CCM inatambua mchango wa wazee katika taifa letu, kuanzia kwenye kupigania uhuru, kujenga utaifa, kujenga uchumi, pamoja na kutunza amani ya nchi yetu baada ya uhuru. Matunda ya Tanzania yenye amani ni matokeo ya mbegu iliyopandwa na nyie wazee wetu,”

“CCM itaendelea kuwaenzi, kuwatunza na kuwaombea umri mrefu zaidi ili sisi vijana tuendelee pia kujifunza historia ya nchi yetu na mengine mengi kutoka kwenu. Ombi letu kwenu wazee wetu ni muendelee kumuombea Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan azidi kuimarisha amani yetu na aendelee kuijenga Tanzania,” Shamira amesema.

Shamira pia amewataka wazee kukiombea chama hicho ili waendelee kufaidi matunda ya maendeleo yanayotekelezwa na serikali likiwemo suala la kuwatengea makao haya ya kuwalea na manufaa mengine mengi ambao wazee wa Tanzania wanapatiwa na serikali.

Mwisho, Shamira alikabidhi mashuka, mchele, sukari, sabuni za kufulia, chumvi, mafuta ya kupikia, na katoni za maji kama sehemu ya kusapoti jitihada zinazofanywa na serikali katika kituo hiko.