“Mshindi atangazwe, Tamisemi msipendelee”

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa(CCM-NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla ameitaka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) kutenda haki kwa vyama vyote vitakavyosikamisha wagombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27,mwaka huu ili kuufanya uwe huru na haki.

Ameongeza kuwa anawaomba atakayeshinda kwa haki atangazwe kwani chama hicho hakihitaji upendeleo wowote na wapo tayari kushindana na kushinda kwa haki.

Advertisement

Makalla amezungumza hayo leo Novemba 8, 2024 akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM katika Ukumbi wa TPA wilayani Temeke ikiwa ni muendelezo wa ziara yake kuzungumzia katika mikoa ya Dar es salaam na Pwani.

“Nitumie nafasi hii kuwaomba TAMISEMI ambao ni wasimamizi wa uchaguzi huu watende haki, kwa CCM na vyama vingine vyote na uchaguzi huu tunaamini utakuwa huru na haki na atakayeshinda kwa haki atangazwe,” amesema Makalla.

Aliongeza kuwa kuhusu pingamizi kwa wagombea zimewekwa kwa vyama vyote hata CCM baadhi ya maeneo wagombea wamewekewa pingamizi na sio kwa vyama vya upinzani tu.

Pia amesema wamejipanga na wanaamini kuwa wamepitisha wagombea wenye sifa na wapo tayari kuanza kampeni ili kuhakikisha ushibdi kwa chama hicho.