Mshindi lugha ya Kichina kuiwakilisha Tanzania

WANAFUNZI 11 kutoka Taasisi ya Kichina katika vyuo vikuu nchini wameonyesha vipaji vyao mbalimbali kwa ajili ya kumpata mshindi atakayekwenda kuwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataia nchini China.

Wanafunzi hao wametoka katika taasisi ya Confucius Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma pamoja na Chuo Kikuu Zanzibar.

Mshauri wa Utamaduni ubalozi wa China nchini Tanzania, Wang Xiping alisema hayo wakati wanafunzi hao walipokuwa wakionyesha vipaji hivyo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Alisema anashukuru kwa wanafunzi na marafiki wanaojali, kuunga mkono na kushiriki kikamilifu katika mashindano ya 22 ya lugha ya kichina kwa wanafunzi wa vyuo, ikiwa ni pamoja na fainali ya 10 ya lugha ya kichina nchini.

Alisema uhusiano wan chi ya China na Tanzania umekuwa mfano wa kuigwa kwani wakuu wan chi hizo mbili mwaka jana walikubaliana kupanua mawasiliano katika Nyanja ya utamaduni na utalii ikiwa ni pamoja na kuendeleza urafiki kati ya nchi hizo mbili.

Awali Naibu Makamu Mkuu wa UDSM anayehusika na taaluma, Profesa Bonaventure Rutinwa alisema anaelewa kuwa mashindano hayo yanahusisha ujumbe tofauti tofauti kutoka vyuo mbalimbali nchini ambao unawasilishwa na wanafunzi kwa njia tofauti tofauti ya kuzungumza lugha ya kichina.

 

Alisema anawahamasisha wanafunzi wengine kusoma kwa bidii na kuwatia moyo wanafunzi wanaopenda kusoma lugha hiyo ya kichina ikiwa ni pamoja na kuonyesha vipaji mbalimbali vikiwemo utamaduni wa kichina.

“Naelewa kuna zaidi ya wachina 10,000 katika viwanda vidogo na vikubwa 500 vilivyopo nchini. Vinahitaji idadi kubwa ya watanzania walio na vipaji mbalimbali na ambao wanaweza kuzungumza kichina,” alisema.

Kwa upande wake mwalimu wa kichina katika taasisi ya Confucius Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sharifu Matumbi alisema mashindano hayo yatawezesha wanafunzi kuzungumza, kuimba, kucheza, kuchora, kuandika na kujibu maswali ya ufahamu.

Habari Zifananazo

Back to top button