Msigwa: Jengo jipya Mtumba usipime!

DODOMA: Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema Jengo jipya la wizara hiyo linalojengwa katika mji wa Serikali Mtumba litakua na eneo la michezo na burudani katika eneo la mbele la jengo hilo, ili kuakisi dhima ya wizara hiyo ya kukuza na kuendeleza Utamaduni, Sanaa na Michezo hapa nchini.

Katibu Mkuu Msigwa amesema hayo Desemba 13, 2023 alipofanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo, ambapo amesema tayari  ameshauriana na Mkandarasi pamoja na mshauri elekezi wa Jengo hilo wafanye maboresho madogo katika eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya maegesho ya magari  liwe eneo la viwanja vidogo vya mpira wa miguu, kikapu na netiboli.

“Nimetembelea mradi, nimeona kazi inaendelea vizuri na sasa tupo asilimia 74, na kwa maelekezo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa lazima tuingie kwenye jengo hili mwezi Januari mwaka 2024, kwahiyo kama wizara tunaendelea  kuhakikisha kazi inafanyika usiku na mchana ili Januari tuhamie” amesema Gerson Msigwa.

Aidha, Amesema vifaa vyote kwa ajili ya kumaliza kazi iliyobaki vimeshawasili eneo la mradi hivyo Mkandarasi ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) anatakiwa kuhakikisha kazi inafanyika kwa haraka na ubora.

Kwa upande wa Mshauri Mwelekezi wa Mradi pamoja na Meneja Mradi wamesema watazingatia ushauri na maelekezo ya Katibu Mkuu huku wakiahidi kukamilisha kazi zilizobaki kwa wakati.

 

Habari Zifananazo

Back to top button