Msuya: JKT, JKU ziunganishwe

DAR ES SALAAM: WAZIRI Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, Cleopa David Msuya ameishauri Serikali kuongeza nguvu katika kutangaza faida za Muungano ili kila mmoja aone haja ya kujivunia miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Msuya ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam, katika mahojiano maalumu na waandishi wa habari nchini kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano, ulioasisiwa Aprili 26, 1964 chini ya Rais wa Zanzibar, hayati Abeid Aman Karume na hayati Mwalimu Julius Nyerere.

“Kuna haja ya kuwa na chombo kimoja cha kuwaunganisha vijana wa bara na visiwani kupata mafunzo ya pamoja ya kujenga taifa ‘National Service’,” ameshauri kiongozi huyo mstaafu.

Advertisement

Ameongeza kuwa, Serikali ione haja ya kuunganisha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) la Tanzania Bara na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) la Zanzibar ili kuwapa fursa vijana kupata mafunzo ya pamoja.

“Nafikiri ni kitu kizuri kwangu binafsi, nanyi vijana naamini mnapaswa kuwa ‘proud’ kuhisi fahari na huu Muungano maana wengi wamefeli ila sisi tunatimiza miaka 60,” ameeleza.

Amesema, hata katika elimu kuna haja ya kuwepo somo la pamoja la Muungano mashuleni.

“Wakati wa Mwinyi (Hayati Alhaj Ali Hassan Mwinyi) ilipitishwa wanafunzi wa shule za msingi kila siku waimbe wimbo ulitungwa na Shaaban Robert nafikiri.

“Anaimba Tanzania, Tanzania nakupenda kwa moyo wote,” amesimulia Waziri Mkuu Mstaafu.