Mtaalamu Lambert Vissot aeleza mafaniko uchimbaji madini

MTAALAMU wa uchimbaji madini kutoka Kampuni ya Madini ya Vito Ruby International Limited, Lambert Vissot amesema kwa miaka ya hivi karibuni kampuni hiyo imekuwa na mafanikio makubwa ya kuuza madini ndani na nje ya nchi.
Vissort maarufu kwa jina la “The Gem Hunter” amezungumza na HabariLeo na kueleza namna wanavyopata soko nje ya nchi hasa kutokana na uwepo wa tawi la kampuni hiyo lililopo Bangkok nchini Thailand.
Mtaalamu huyo wa ugunduzi wa madini ya spinel nyekundu na pinki amesema umoja na mshikamano wa pamoja na maono ya baadhi ya viongozi imekuwa sababu ya mafaniko hayo kwa miaka mingi.
“Mafanikio ni makubwa kiukweli siwezi kueleza yote ila tumekuwa na wakati mzuri sana nchini Thailand kama unavyofahamu tuna tawi letu linalofanya kazi kule, hivyo tunajivunia sana hakika,” amesema Vissot.
“Kampuni imeendelea kuimarka kwa kiasi kikubwa sana, wafanyakazi wamekuwa wakijitoa kwa kiwango cha juu, hivyo nadhani ni sababu ya kampuni kuendelea kufanya vizuri,” ameongeza.
Vissot raia wa Ufaransa amesema sifa yake kubwa ni kupata madini bora kutoka katika maeneo yenye ubora wa kipekee ambayo yanawezesha kutengeneza bidhaa mbalimbali ulimwenguni.
Amesema maarifa makubwa aliyonayo na ustadi wake vinaendelea kuimarisha nafasi ya Ruby International katika sekta ya kimataifa ya uuzaji na ununuzi wa madini ya vito.
Kufikia Mei 7, 2024 vijana zaidi ya 525 wa Kitanzania walikuwa wamejipatia nafasi za kazi, ambao kati ya hao 125 walikuwa na ajira za kudumu na wengine 400 walikuwa wafanyakazi wa muda katika kampuni hiyo.
Kampuni hiyo yenye makao makuu yake Ulanga mkoani Morogoro, ambayo pia inahudumu Bangkok nchini Thailand ilianzishwa mwaka 2014, ambapo mpaka sasa ni miaka 11.
Kampuni ya Ruby International Limited inamilikiwa na Mbunge wa Jimbo la Ulanga mkoani Morogoro, Salim Hasham.