“Mteja atafidiwa pesa taslimu”

BARAZA la Ushauri na Utetezi wa Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC) limezitaka mamlaka na taasisi za huduma hizo kuzingatia kanuni, taratibu na haki ya wateja wanapotoa huduma.

Ofisa Tawala Msaidizi kutoka EWURA CCC, Wadi Omari amesema hayo jana mbele ya waandishi wa habari katika viwanja vya maonyesho ya sita ya kimataifa ya teknolojia ya madini mjini Geita.

Ofisa huyo amesema mbali na kutoa huduma ana wajibu wa kutambua mteja wake ana haki ya kupewa huduma sahihi, stahiki na kwa wakati pindi anapolipia na inapotokea dharura afahamishwe.

Ametolea mfano mtu anapolipia huduma ya umeme anapaswa ndani ya siku 30 za kazi awe ameunganishiwa, na endapo kuna changamoto basi mteja aarifiwe vinginevyo ni ukiukaji wa haki.

“Huduma hizi (maji na nishati) ni huduma kiritimba, kwa maana hazina mbadala, kwa maana kwamba binadamu anapohitaji maji anahitaji maji, anapohitaji umeme anahitaji umeme.”

Amesema , kanuni ya utoaji huduma inaelekeza iwapo mtoa huduma atachewesha kuunganisha huduma ya maji na umeme atapaswa kumfidia mteja wake kwa pesa taslimu ama kihuduma.

“Kwa kipindi hiki katika siku ambazo tupo hapa, tumekusanya malalamiko zaidi ya 15, ambapo malalamiko mengi yamekuwa yakitokea kwenye sekta ya maji, umeme pamoja na mafuta.

“Tuna malalamiko ambayo yanatokana na kuchelewa kuunganishwa huduma, kwenye sekta ya umeme kwa mfano tangu kipindi kile watu wanalipa Sh 27,000/= tunao watu mpaka sasa hawajaunganishwa.

Ameahidi EWURA CCC inaendelea kuwasiliana na mamlaka husika ili kutatua malalamiko huku akiwataka watanzania kufuata taratibu za utoajia malalamiko badala ya kubaki na manung’uniko nyumbani.

“Sisi tunasema huduma bora ni haki yako, haki yako ni huduma bora, kwa amaan ni kwamba unapopata huduma ya maji lazima upate maji safi na salama, na yapatikane kadri vie unavyolipia.”

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button