KUELEKEA uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27,2024, Mkuu wa Wilaya wa Tandahimba mkoani Mtwara, Michael Mtenjele amezindua zoezi la uandikishaji wa daftari la wapiga kura kwa wakazi wa kitongoji cha Mihuru kilichopo wilayani Tandahimba mkoani humo.
Akizungumza leo wilayani humo wakati wa uzinduzi huo, Mtenjele ametoa wito kwa wananchi wote wilayani humo wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari hilo la wakazi lililopo katika maeneo yao.
“Wananchi wahakikishe wanaenda kujiandikisha kwa wakati ili waweze kuendelea na majukumu mengine na kuepuka msongamano siku za mwisho,” amesema Mtenjele.
Aidha ametoa rai kwa waandikishaji wa zoezi hilo kuwa, wao wamepewa mafunzo kwa wakati hivyo inatakiwa wafanye kazi kwa muda ambao umewekwa na wasimamizi wa uandikishaji katika maeneo yote na watoe huduma hiyo kila wakati ili mtu anayekuja aweze kupata huduma kadri inavyowezekana.
Hata hivyo kwa upande wa wazee, wajawazito na wagonjwa wamepewa fursa ya kupewa kipaumbele wajiandikishe ili waende wakapumzike au wakaendelee na majukumu yao.
Msimamizi mkuu wa uchaguzi katika halmashauri hiyo, Mariam Mwanzalima amesema wamejipanga vizuri na wanatarajia kuandikisha watu zaidi ya 100,000.
SOMA: Uboreshaji daftari wapiga kura kuzinduliwa leo
Hata hivyo wana jumla ya vituo 650 vya uandikishaji katika maeneo yote na tayari wamehamasisha vya kutosha na hata waandikishaji na mawakala wote wa vyama vya siasa wameshapatiwa mafunzo na wamehapa.
“kwa upande wasimamizi wote wazingatie mafunzo waliyopewa kwa umakini na uhadilifu na natoa wito kwa wana Tandahimba kujitokeza kwa wingi ili waweze kujiandikisha kwenye daftari la kupiga kura katika uchaguzi huo”
Baadhi ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali wilayani humo wametoa wito kwa wananchi wenzao waweze kushiriki zoezi hilo kwa sababu ni haki ya kikatiba na waweze kuchagua viongozi bora na waadilifu.