KIGOMA: Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Julai 20, 2024 anazindua uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, katika uwanja wa Kawawa, mkoani Kigoma.
Uzinduzi huo unaashiria kuanza kwa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura nchini nzima. Mikoa ambayo inaanza uboreshaji wa daftari hilo Julai 20, 2024 hadi Julai 26, 2024 ni Kigoma, Katavi na Tabora na baadaye mikoa mingine itafuata.
Kauli Mbinu ya uboreshaji ni: ‘Kujiandikisha kuwa Mpiga Kura ni Msingi wa Uchaguzi Bora.’
SOMA: INEC: Waandishi kiungo muhimu elimu ya mpiga kura
Asasi zilizopata kibali cha uangalizi wa uboreshaji wa daftari mwaka 2024/2025 NI 33.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imeruhusu wapiga kura waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, wanaotaka kuboresha au kuhamisha taarifa zao kutoka jimbo au kata moja kwenda jimbo au kata nyingine kutumia simu ndogo za kitochi au kiswaswadu kuanzisha mchakato wa uboreshaji wa Daftari.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Kailima Ramadhani ilisema uamuzi huo wa Tume umetokana na maoni ya wadau wa uchaguzi.
“Tume imefanyia kazi maoni na ushauri huo (wa wadau) na kuanzia tarehe 20 Julai, 2024 watu wote wenye simu za kawaida (maarufu kama kitochi au kiswaswadu) na watahitaji kuboresha au kuhamisha taarifa zao, watapata huduma hiyo kwa kupiga USSD Code *152*00# na kubonyeza namba 9 kisha kuendelea na hatua zingine kama itakavyokuwa inaelekezwa kwenye simu husika,”ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Imefafanua kuwa mpiga kura anayetumia njia hii atapokea namba maalum (token) kupitia simu yake kisha atalazimika kwenda na namba hizo kwenye kituo anachotarajia kutumia kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ili kukamilisha mchakato na kupewa kadi mpya.
Katika hatua nyingine, Tume imetoa taarifa kwa umma kuhusu kuanza rasmi kwa kituo cha huduma kwa mpiga kura (Call Centre) kinachoanza kutoa huduma kuanzia tarehe 18 Julai, 2024.
Huduma hiyo ni ya bure na itatolewa kwa saa 14 kila siku kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 2:00 usiku.
“Kupitia kituo hiki wananchi watapata fursa ya kupiga simu bila malipo kupitia namba 0800112100 na kupata majibu au ufafanuzi wa maswali au jambo lolote linalohusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Hivyo, wananchi wote mnakaribishwa kutumia huduma hii kwa kipindi chote cha uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.