Mtuhumiwa wa mauaji mwili wake wapatikana

JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga limesema katika uchunguzi wa awali uliofanyika kwenye mwili uliopatikana ukiwa umeharibika Oktoba 7,2024 katika Msitu wa Galanos Wilaya na jijini la Tanga umebainika ni mwili wa Ali Mohamed maarufu Bagdad, 60, anayetuhumiwa kumnyonga mkewe na dada wa kazi Septemba 30 mwaka huu.
Marehemu Ali Mohammed aliyekuwa mkazi wa barabara ya nne jijini Tanga, alikuwa akitafutwa kwa tuhuma za kumuua mke wake Saira Ali Mohamed na mfanyakazi wao wa ndani kwa kuwanyonga kisha kuwatoboa macho Septemba 30, 2024.

SOMA: Ajali yauwa wanne,15 wakijeruhiwa Tanga
Katika taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga jana imeeleza kuwa uchunguzi zaidi unaendelea kwa kushirikisha wataalam wa uchunguzi wa vifo ili kubaini kifo chake kimesababishwa na kitu gani.
Aidha, Jeshi la Polisi linaendelea kuwaasa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwani kufanya hivyo kunasababisha madhara zaidi na ni kinyume na sheria za nchi.
SOMA: OCD’s Tanga wafundwa



