MUCE yafafanua mafanikio ya serikali ya Dk Samia katika elimu

IRINGA: Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) kimepongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa ulioleta mageuzi ya kweli katika elimu ya juu kupitia Mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET), unaotekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.
Akizungumza chuoni hapo wakati wa maadhimisho ya kumbukizi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rasi wa MUCE, Prof. Method Samwel Semiono, alisema mradi huo ni uthibitisho wa dhamira ya serikali ya kuboresha ubora wa elimu na kuandaa wahitimu wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.
“Mageuzi haya hayajawahi kushuhudiwa katika historia ya chuo chetu. Tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa maono makubwa yanayobadilisha taswira ya elimu ya juu nchini,” alisema Prof. Semiono.
Mradi wa HEET unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2021 hadi Juni 2026, umewezesha Serikali kuwekeza chuoni hapo zaidi ya Sh bilioni 18.6 kwa ajili ya kuboresha mitaala, ujenzi wa miundombinu, kuendeleza rasilimali watu, kuboresha matumizi ya TEHAMA, kuimarisha elimu jumuishi na usawa wa kijinsia na kuimarisha uhusiano kati ya sekta binafsi na tasnia.
Kupitia Kamati ya Ushauri wa Viwanda, alisema MUCE imeingia mikataba ya ushirikiano na taasisi mbalimbali zikiwemo TPHPA na Sao Hill Industries, kwa lengo la kufanya tafiti na mafunzo yanayolenga sekta za kilimo, misitu na viwanda.
“Ushirikiano huu unasaidia wanafunzi kupata uzoefu wa vitendo sambamba na mahitaji ya soko,” alisema.
Kupitia mradi wa HEET, Prof Semiono alisema MUCE imefanya mapitio ya mitaala mitano ya zamani na kuandaa mitaala mipya 30, ikiwemo saba za uzamili (Masters) na mbili za uzamivu (PhD).
Alisema idadi ya programu za uzamili imeongezeka kutoka tano hadi 14, huku udahili wa wanafunzi ukitarajiwa kufikia zaidi ya 10,000 katika miaka michache ijayo.
Mitaala hiyo imeandaliwa kwa kushirikisha sekta binafsi na wadau wa ajira, ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa wabunifu, wanaojiajiri na kuchangia moja kwa moja katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Katika upande wa miundombinu, MUCE imepokea zaidi ya Sh bilioni 15.3 kwa ajili ya ujenzi wa majengo manne makubwa, yakiwemo bweni la wanafunzi, maabara ya fizikia, kituo cha elimu maalumu na midia anuai, pamoja na jengo la sayansi lenye maabara za kisasa.
Meneja wa Kitengo cha Miliki na Usimamizi wa Ujenzi, Geofrey Ngelime, alisema hosteli hiyo mpya yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 152 itapunguza changamoto ya malazi hasa kwa wasichana na wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Kupitia mradi wa HEET, MUCE imetandaza nyaya za fibre optic, kuimarisha mifumo ya intaneti, na kuanzisha mfumo wa masomo kwa njia ya mtandao.
Meneja wa TEHAMA wa chuo hicho, Sebastian Majimoto, alisema mfumo huo unamwezesha mwanafunzi kusoma, kuuliza maswali, na kufanya mitihani akiwa popote.
“Elimu sasa haina mipaka. Dunia inaelekea kwenye teknolojia, na sisi kama chuo tupo mstari wa mbele kuhakikisha mwanafunzi anapata elimu bora hata akiwa mbali,” alisema Majimoto.
Serikali pia imewezesha watumishi 31 wa MUCE kupata mafunzo ya shahada za uzamili na uzamivu ndani na nje ya nchi, huku wengine wakipata mafunzo mafupi katika ufundishaji wa kidijitali na tafiti za kisayansi.
Mhadhiri wa chuo hicho, Dk Baraka Luvanga, ambaye amenufaika na ufadhili wa HEET, alisema elimu bora ni nguzo ya uchumi imara.
“Kupitia HEET nilipata nafasi ya kusoma shahada ya uzamivu na sasa narudi nikiwa na maarifa mapya. Uwekezaji huu ni msingi wa maendeleo endelevu ya elimu nchini,” alisema Dk Luvanga.
Pamoja na hayo MUCE imeanzisha Dawati la Masuala ya Kijinsia na Kitengo cha Watu Wenye Mahitaji Maalum, pamoja na kujenga kituo maalum chenye vifaa vya kisasa kama lifti, bajaji maalum, na vifaa vya TEHAMA kwa wanafunzi wenye ulemavu.
Mtaalamu wa upimaji masikio na lugha ya alama, Joseph Paul, alisema kituo hicho kitawawezesha wanafunzi wenye changamoto za usikivu, uoni na viungo kusoma katika mazingira rafiki.
“Ni hatua kubwa ya kuhakikisha kila mwanafunzi anapata elimu bila vizuizi. Hii ndiyo maana halisi ya elimu jumuishi,” alisema Paul.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa MUCE, Musa Mgema, alisema wanafunzi wameanza kuona matokeo ya uwekezaji wa serikali kupitia HEET, hususan kwenye upande wa makazi na mazingira ya kujifunzia.
“Hosteli mpya zitatatua changamoto tulizokuwa tunakabiliana nazo kwa muda mrefu. Wanafunzi wengi sasa wataishi katika mazingira salama na bora zaidi,” alisema Mgema.
Make money while staying at home and working online. I just received $23,783 for my work last month, and I was doing this part-time. This year, I plan to earn even more, and I believe you can also make extra cash from this job. To join right now, follow the details on this website.
Open This… http://Www.Work99.Site