Mufti ahimiza ushirikiano, amani Uchaguzi Mkuu

MUFTI na Shehe Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir amewataka Watanzania kuendelea kuonesha ushirikiano, umoja na upendo sambamba na kuliombea taifa ili Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 uishe kwa amani na utulivu.
Katika salamu zake za Idd El Adha kwa Waislamu wote nchini, Mufti Zubeir kupitia Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), alisisitiza umuhimu wa mshikamano wa kitaifa na dua kwa taifa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Akizungumza na gazeti la HabariLEO, Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Bakwata, Said Mpeta alisema Swala ya Idd kitaifa itaswaliwa leo katika Msikiti wa Mfalme Mohamed VI uliopo Makao Makuu ya Bakwata, Kinondoni, Dar es Salaam kuanzia saa 1:30 asubuhi, ikifuatiwa na Baraza la Idd.
Mpeta alibainisha kuwa mgeni rasmi katika baraza hilo anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye pia ataongoza waumini katika kuswali Swala ya Idd.
Kwa upande wa Zanzibar, Swala ya Idd El Adha itaswaliwa Wilaya ya Kati katika Msikiti wa Ijumaa uliopo Bambi kuanzia saa 1:15 asubuhi, kisha Baraza la Idd kufanyika katika Viwanja vya Shule ya Suza Tunguu, Unguja.
Sikukuu ya Idd El Adha huadhimishwa baada ya mahujaji kukamilisha Ibada ya Hijja katika mji mtakatifu wa Makka nchini Saudi Arabia, ikiwa ni moja ya nguzo tano za dini ya Kiislamu.