Mufti ateua mshauri wa dini, uchumi

DODOMA; SHEHE Mkuu wa Tanzania, Mufti Abubakar Zubeir amemteua Ismail Dawood kuwa mshauri wake katika masuala ya dini, uchumi, maendeleo na jamii.
Dawood ni msimamizi mkuu wa msikiti wa Nunge wa jijini Dodoma.
Akimkabidhi barua kwa niaba ya mufti mwishoni mwa wiki katika msikiti wa Nunge, Naibu Kadhi Mkuu, Shehe Ally Ngeruko alisema sababu ya uteuzi huo ni kutokana na familia ya Dawood kuleta umoja na mshikamano katika masuala ya dini.
Wengine waliohudhuria makabidhiano hayo ni pamoja na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, Katibu wa Sekretarieti ya Baraza la Ulamaa na Mratibu wa Ofisi ya Mufti, Shehe Swedi Twaibu Swedi na Waumini wa msikiti wa Nunge.
“Familia hii inajulikana kwa kujitoa kwa ajili ya Allah (Mwenyezi Mungu) ndio maana Mufti akanituma nije hapa kukabidhi hii barua ya uteuzi,” alisema Sheihe Ngeruko.
Ulega alisema uteuzi huo ni heshima kwa msikiti wa Nunge na Waislamu wa Mkoa wa Dodoma.
“Maana akipata yeye tumepata waumini wote, tumshukuru Mufti kwa uteuzi huu maana nafasi hizi hutolewa kwa sababu maalumu na mtoaji huamua yeye kwa vigezo vyake yeye anavyovijua, tunamshukuru Mufti,” alisema.
Dawood alisema uteuzi huo anautoa kwa familia yake na wazazi wake ambao walimlea katika mazingira ya kujitolea kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
“Kwa niaba ya familia yangu natoa shukurani kubwa sana hii ni heshima sio ya kwangu ni ya familia, mimi sistahili ila wazazi wangu ndio waliofanikisha hili, naomba watoto wangu na Wajukuu zangu wafuate nyayo zangu,” alisema.
Aliongeza: “Naomba Waislamu waliopo Dodoma waniunge mkono wafanye juhudi kuanzisha Chuo Kikuu Cha Waislamu wote tushirikiane, nawashukuru sana”.