Muhas waandaa kambi uchunguzi magonjwa ya moyo

DAR ES SALAAM: CHUO Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimesema kimeandaa Kambi Maalum ya Afya ya Moyo kuanzia Mei 21 hadi Mei 22, 2025 ambapo wananchi watapata fursa ya kufanyiwa uchunguzi wa awali wa viashiria vya moyo, uchunguzi wa visababishi vya magonjwa ya moyo.
Pia watapata elimu na ushauri kuhusu afya ya moyo, matumizi sahihi ya dawa za magonjwa ya moyo
na huduma saidizi kwa wagonjwa wa moyo ambapo zoezi hilo litaanza saa 3 asubuhi hadi saa 11 jioni eneo la Kampasi ya Mloganzila.
Akizungumza na waandishi wanahabari leo Mei 19, Makamu Mkuu wa Muhas, Profesa Appolinary Kamuhabwa amesema kambi hiyo ni sehemu ya shughuli mahususi zinazoadhimisha uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Mradi wa Kituo cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu Afrika Mashariki, ambao utafanyika Mei 23, 2025.
Amesema kambi hiyo yenye kauli mbiu ya “Linda Afya ya Moyo Wako” inakuja baada ya mafanikio makubwa ya awamu ya kwanza iliyojumuisha ujenzi wa jengo la kufundishia (Multipurpose Building) na mafunzo kwa wataalamu wa afya.
“Awamu ya pili inalenga kujenga hospitali ya kisasa ya moyo, kuendeleza mitaala ya kitaaluma, kufanya tafiti za kina kuhusu kinga, tiba na ukarabati wa magonjwa ya moyo, pamoja na programu za kijamii ‘Community Outreach Programs’,” amesema Prof Kamuhabwa.
Amesema kituo hiko ni sehemu ya mpango wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa kuanzisha vituo vya umahiri kwenye fani tofauti, na Tanzania kupitia MUHAS imepewa dhamana ya kuongoza katika nyanja ya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.
Aidha, mgeni rasmi katika uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Mradi huo atakuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.



