MUHAS wahitimisha mafunzo wataalamu 27 wa ‘dialysis’

DAR ES SALAAM: Washiriki 27 kutoka kada za madaktari, maofisa tabibu na wauguzi wamehitimu Mafunzo ya Muda Mfupi ya Hemodialysis, awamu ya tano, yaliyotolewa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kwa lengo la kuimarisha ubora wa huduma kwa wagonjwa wenye magonjwa ya figo nchini.
Mafunzo hayo yaliyoanza Septemba 14, 2026, yamehitimishwa leo, Oktoba 23, 2026, yakiwa sehemu ya juhudi za MUHAS za kuongeza uwezo wa kitaaluma wa watoa huduma za afya, hususan katika matibabu ya hemodialysis yanayotumika kusaidia wagonjwa ambao figo zao hazifanyi kazi ipasavyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Msajili wa Vituo Binafsi vya Kutolea Huduma za Afya, Meshack Shimwela, amesema mafunzo hayo ni hatua muhimu katika kuboresha mfumo wa utoaji huduma za afya na kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wagonjwa.

Amesema idadi ya vituo vinavyotoa huduma za hemodialysis nchini imefikia 77, ambapo 29 vinamilikiwa na Serikali, huku vingine vikiwa chini ya watoa huduma wengine.
Shimwela amewataka wahitimu kuendelea kushirikiana na kubadilishana taarifa na uzoefu ili kuimarisha ujuzi wao na kuboresha huduma kwa wagonjwa.

“Lazima tushirikiane kupeana taarifa. Kuhitimu hakumaanishi kwamba mmemaliza kila kitu. Naomba niseme kwamba mpaka leo sisi bado tunauliza maswali,” amesema Shimwela.

Kwa upande wake, Profesa Emmy Meta, Mkurugenzi wa Elimu Endelevu na Maendeleo ya Kitaaluma wa MUHAS, amesema mafunzo hayo yameendeshwa mara tano tangu yalipoanzishwa, huku jumla ya wataalamu 105 wa afya wakinufaika.
Amesema wanufaika hao ni madaktari, maofisa tabibu na wauguzi kutoka maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, Dodoma, Njombe, Lindi, Mtwara, Mara, Mwanza, Zanzibar, Iringa na Singida.

Profesa Meta amesema pamoja na kutoa mafunzo, ni muhimu kufuatilia wahitimu na kutathmini namna wanavyotumia kwa vitendo ujuzi walioupata katika vituo vyao vya kazi.
Amesema baadhi ya wahitimu wameeleza kuwa mafunzo hayo yamewasaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kuboresha ubora wa huduma wanazowapatia wagonjwa.

Katika awamu ya tano, washiriki hao walijumuisha madaktari wawili, maofisa tabibu 17 na wauguzi wanane. Walitoka Dar es Salaam, Arusha, Morogoro na Kagera.

Mafunzo hayo yalihusisha nadharia zilizofundishwa katika madarasa ya MUHAS, mazoezi ya ujuzi katika maabara ya vitendo ya Multi-User Clinical Skills Lab ya chuo hicho, pamoja na mafunzo ya vitendo ya kliniki yaliyofanyika kwa wiki tano.
Mafunzo ya vitendo yalifanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, kampasi za Upanga na Mloganzila, pamoja na vituo vitano vya huduma za dialysis vinavyoendeshwa na Africa Healthcare Network (AHN) jijini Dar es Salaam.

Vituo hivyo ni Shree Hindu Mandal Hospital – Dialysis Center, Posta; Cardinal Rugambwa Hospital (CRH) – Dialysis Center, Ukonga; Comprehensive Community Based Rehabilitation in Tanzania (CCBRT) – Dialysis Center, Msasani; E.M. Hospital – Dialysis Center, Kigamboni; na Shree Hindu Mandal Super Specialized Polyclinic – Dialysis Center, Kunduchi.
Katika mafunzo hayo, washiriki walijifunza kanuni za kisayansi za hemodialysis na uendeshaji wa mashine za dialysis, ufuatiliaji wa hali za wagonjwa wakati wa matibabu na utambuzi wa mapema wa matatizo yanayoweza kujitokeza.

Pia, walipata ujuzi kuhusu utunzaji wa njia za kufikia mishipa ya damu kwa ajili ya dialysis, ikiwemo arteriovenous fistula na central venous catheter, pamoja na udhibiti wa maambukizi na kuzingatia taratibu za usalama wa wagonjwa.
Profesa Meta amesema tathmini ya mara kwa mara itasaidia kubaini mafanikio ya mafunzo hayo, changamoto zinazowakabili wahitimu na maeneo yanayohitaji kuboreshwa ili kuhakikisha ujuzi waliopata unachangia kuimarisha huduma za afya nchini.



