MUHAS watakiwa kujenga uwezo ufanyaji utafiti
![](https://habarileo.co.tz/wp-content/uploads/2023/11/WhatsApp-Image-2023-11-16-at-17.58.05-780x470.jpeg)
CHUO Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS), kimetakiwa kujenga zaidi uwezo wa ufanyaji tafiti mbalimbali zinazohusiana na masuala ya afya, ili kuimarisha huduma ya afya nchini.
Hayo yamesemwa leo Novemba 16, 2023 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Peter Msofe kwa niaba ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda katika kongamano la Maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa MUHAS mwaka 1963.
Amesema ili kuboresha huduma za afya nchini kuna haja ya watafiti na wataalamu kuendelea kutafuta njia za kuimarisha huduma hiyo licha ya changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo.
“Utaalamu katika kutafuta njia za kuboresha huduma za afya ni muhimu kwa Watanzania wote.
Nawasihi kuendelea kufanya tafiti lakini pia kuyatumia matokeo haya ya kitafiti kikamilifu, ili kusaidia serikali kuboresha huduma ya afya kwa wananchi, “amesema Msofe.
Amesema, MUHAS imezalisha zaidi ya wataalumu 20, 000 wanaopigania afya na ustawi wa Watanzania, ni sehemu ya tafiti nyingi ambazo zimetumika kuleta matokeo.
Kwa upande wa Kaimu Mkuu wa Chuo cha MUHAS , Profesa Apolinary Kamuhabwa amesema jumla ya tafiti 136, zinaendelea kufanywa zikijikita katika maradhi ya kuambukiza, yasiyoambukiza pamoja na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Uviko-19.
Miradi hiyo inayotekelezwa na Muhas pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ni sehemu ya utekelezaji wa afua, mbalimbali kudhibiti magonjwa kama virusi vya Ukimwi, malaria, kifua kikuu, saratani, moyo na yale yasiyoambukiza yaliyotajwa kuongezeka kwa kasi.
Amesema kupitia kongamano hilo la miaka 60 ya MUHAS watajadili ilipotoka, ilipo na inapoelekea, lengo ni kutatua changamoto mbalimbali za Watanzania na kuboresha mifumo ya afya, ujuzi na weledi wa wataalamu wa afya.