Muhimbili waja kivingine wagonjwa NHIF

DAR ES SALAAM: Kufuatia baadhi ya Hospitali binafsi kusitisha huduma kwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH),imetangaza mpango wa dharura kwa wagonjwa ambao ni wanachama wa mfuko huo kuanzia leo Machi Mosi, 2024.

Akizungumza leo Mkurugenzi wa Muhimbili, Prof Mohamed Janabi amesema wametoa mpango huo wa dharura, ili wanachama waweze kuwa na mwendelezo wa huduma hizo.

Amesema MNH imefanikiwa kuhamia kwenye kitita kipya cha mafao cha mwaka 2023 kilichopendekezwa na NHIF, ambapo huduma zinaendelea kutolewa.

 

Amesema, Hospitali imeongeza muda wa kuhudumia wagonjwa katika kliniki zote za Upanga kupitia vyumba 75 vya kuona wagonjwa na vyumba vya kuona wagonjwa 59 viliyopo Mloganzila kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa nne usiku au mpaka mgonjwa wa mwisho atakapomaliza kuonwa na daktari.

“Tunajua kuna wagonjwa waliopangwa kufanyiwa upasuaji, tunavyo vyumba 18 vya upasuaji Upanga na Mloganzila vyumba vya upasuaji 13,” amesema Prof Janabi na kuongeza:

“Kwa wagonjwa wenye tatizo la figo wanaohitaji kusafishwa damu, Upanga tunazo mashine 47 za kutoa huduma hiyo na tumeongeza zamu (sessions) za kutoa huduma hiyo katika mzunguko wa saa nne wa kila zamu kutoka tatu hadi nne kwa Upanga na Mloganzila ambapo kuna mashine 12 tumeongezea mizunguko kutoka miwili hadi minne na muda unaobaki ni wa kufanya matengezo kinga pamoja na usafi wa mashine hizo,” amesema.

Amesema MNH kama mmoja wa watoa huduma wakubwa nchini, nayo itaendelea kufuatilia utendaji wa kitita hicho ili kubaini changamoto zitakazojitokeza na kuziwasilisha katika mamlaka husika.

Habari Zifananazo

Back to top button