JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linawashikilia mume na mke, wakazi wa Mtaa wa Mji Mwema Manispaa ya Songea kwa tuhuma za kuiba mtoto mwenye umri wa miezi 11 (jina limehifadhiwa).
Pia, jeshi hilo linawatafuta wanawake wengine wawili wanaotuhumiwa kushiriki kuiba mtoto huyo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chillya alisema tukio hilo ni la Novemba 4, 2024 saa 8:00 mchana.
Kamanda Chillya alisema mtoto huyo ni wa mfanyabiahara wa saluni, Gabriela Hinju (24) Mkazi wa Mji Mwema Manispaa ya Songea.
Kwa mujibu wa kamanda, mwanamke huyo alitoa taarifa katika Kituo Kikuu cha Polisi Wilaya ya Songea kuhusu kuibwa kwa mtoto wake.
Gabriela alieleza kwamba siku ya tukio, mwanamke aliyemtambua kwa sura alifika saluni hapo kwa ajili ya kupata huduma ya kusukwa na kipindi yupo kwenye foleni, mtoto wa msusi huyo alikuwa analia ndipo mwanamke huyo akaomba ambebe ili akambembeleze nje, kisha akatokomea naye kusikojulikana.
Alisema baada ya tukio, walianza ufuatiliaji mtuhumiwa na mtoto huyo na juzi walimpata mtoto akiwa ndani ya chumba cha fundi cherehani, Janeth Nombo (25) mkazi wa Mji Mwema Manispaa ya Songea anayetuhumiwa kumuiba saluni na kumficha.
“Mtuhumiwa amehojiwa na amekiri kumuiba mtoto huyo akishirikiana na wenzake wawili ambao majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi na kwamba sababu ya kufanya kitendo hicho ni kuwa wameishi na mume wake kwa miaka saba bila kupata mtoto ndipo akaamua kutekeleza azma hiyo ili amdanganye mumewe kuwa amejifungua,” alisema.
Aidha, kamanda alitoa wito kwa wazazi na walezi mkoani humo kulinda na kuwatunza watoto na si kuwakabidhi kwa watu wasiowafahamu ili kuepuka matukio ya wizi wa watoto.
Kwa upande wake, baba wa mtoto huyo, James Nyoni ameshukuru Jeshi la Polisi kwa ushirikiano mkubwa waliompatia pamoja na wananchi na kusaidia kupatikana kwa mwanaye akiwa na afya njema.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Gabriela amewataka wanawake kuacha uzembe akisisitiza wasiwaamini watu na kuwakabidhi watoto.
Kwa upande wake, Raymond Mbilinyi mume wa mwanamke anayedaiwa kuiba mtoto huyo alisema, alidanganywa na mkewe kuwa amejifungua mtoto njiti, hivyo wazazi wanamsaidia kumtunza kumbe alikuwa ameiba na kumficha hadi alipokamatwa na polisi kwa tuhuma hizo.