Muswada wa marekebisho sheria mbalimbali wapitishwa
DODOMA;BUNGE limepitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.2) wa Mwaka 2023, uliowasilishwa mapema asubuhi leo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji, Dk Eliezer Feleshi .
Miongoni mwa sheria zilizowasilishwa kufanyiwa marekebisho ni Sheria ya Nguvu ya Atomu Sura ya 188, Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusu Umiliki wa Mali na Rasilimali Asilia, Sura ya 449.
Nyingine ni Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu masharti hasi katika mikataba Mali na Rasilimali Asilia na Sheria ya Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda, Sura ya 159.
Kuhusu marekebisho ya Sheria ya Nguvu ya Atomu Sura ya 188, Jaji Feleshi amesema kifungu cha 4 kinarekebishwa ili kuongeza mawanda ya udhibiti kwa kushusha viwango vya vyanzo mbalimbali vya mionzi inayosimamiwa na sheria hiyo.
“Lengo la marekebisho haya ni kudhibiti mmuliko wa mionzi unaotokana na Madini na Viasili vya Mionzi ya Asili (NORMs)” amesema Jaji Feleshi.