Muungano wa bodi kuleta mageuzi sekta ya mifugo

IRINGA: Serikali imetangaza mpango wa kuunganisha Bodi ya Maziwa na Bodi ya Mifugo ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa sekta ya mifugo na maziwa nchini, hatua inayotarajiwa kuleta mageuzi katika uzalishaji, usindikaji na masoko ya maziwa kwa manufaa ya wafugaji na uchumi wa taifa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Wiki ya 29 ya Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa Kitaifa uliofanyika katika Uwanja wa Mwembetogwa mkoani Iringa, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, alisema hatua hiyo inalenga kupunguza urudufu wa majukumu na kuongeza ufanisi wa taasisi zinazohudumia sekta hiyo muhimu.
Alisema sekta ya maziwa ina nafasi kubwa ya kuchangia ukuaji wa uchumi wa wafugaji na taifa kwa ujumla, lakini inahitaji mifumo madhubuti ya usimamizi, uwekezaji katika miundombinu na ushirikiano wa wadau wote.

“Tunapaswa kuimarisha mnyororo mzima wa thamani wa maziwa kuanzia uzalishaji, ukusanyaji hadi usindikaji ili kuhakikisha wafugaji wananufaika moja kwa moja,” alisema Waziri Bashiru.
Aidha, alibainisha kuwa baadhi ya viwanda vya usindikaji wa maziwa vinakabiliwa na changamoto za kifedha na uendeshaji, hali inayosababisha kuchelewa kwa malipo kwa wafugaji, na kusisitiza haja ya maboresho ya kiutendaji katika sekta hiyo.
Alitaja pia umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika kuelimisha jamii kuhusu lishe bora kupitia maziwa, akisema bado kuna pengo kubwa la uelewa kuhusu umuhimu wake hususan kwa watoto.

Katika hatua nyingine, wadau wa sekta hiyo wamesema wafugaji wadogo wanaendelea kunufaika na kuimarika kwa masoko rasmi, miundombinu ya ukusanyaji na huduma za ugani, hali inayosaidia kuongeza kipato vijijini.
Kwa mujibu wa Heifer International Tanzania, zaidi ya kaya milioni 1.3 zimefikiwa na programu za kuboresha kilimo na ufugaji, huku zaidi ya vyama 160 vya wafugaji vikiimarishwa ili kuongeza ushirikiano na upatikanaji wa masoko.
Kupitia Mradi wa TI3P, vituo 41 vya ukusanyaji wa maziwa vimeanzishwa vyenye uwezo wa kupokea zaidi ya lita 108,000 kwa siku, hatua inayosaidia kuongeza ufanisi wa mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.

Aidha, zaidi ya watoa huduma za ugani 1,200 wamepatiwa mafunzo ili kuboresha huduma za afya ya mifugo vijijini.
- Wiki ya Maziwa Kitaifa huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha uzalishaji, usindikaji na matumizi ya maziwa pamoja na kuonesha mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa taifa.



