MV New Mwanza Kufungua fursa utalii Afrika Mashariki

MWANZA: MKURUGENZI wa Bodi ya Utalii nchini (TTB), Ephraim Mafuru, amesema Tanzania inaendelea kuweka historia katika uwekezaji wa miundombinu ya usafiri, usafirishaji na utalii barani Afrika, kufuatia uzinduzi wa meli kubwa ya kisasa ya MV New Mwanza jijini humo.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo ulioongozwa na Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba Januari 23, 2026, Mafuru amesema Meli hiyo ni ya kwanza kwa ukubwa katika Bara la Afrika ukilinganisha na meli nyingine zinazofanya kazi katika maji baridi hususani maziwa.

Amesema Tanzania imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika kujenga na kuzindua meli hiyo kubwa yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 kwa wakati mmoja, magari madogo 20, magari makubwa matatu pamoja na tani 400 za mizigo.
“Ukizungumza tani 400 za mizigo, ni sawa na kubeba magari makubwa ya aina ya semi trailer takribani 13 kwa wakati mmoja. Aidha, urefu wa meli hii ni mita 92, sawa na urefu wa uwanja mmoja wa mpira wa miguu,” amesema Mafuru.
Ameongeza kuwa Serikali, imetumia kiasi cha zaidi ya sh. bilioni 120, kujenga meli hiyo kwa ajili ya kuimarisha usafirishaji wa abiria na mizigo katika Ziwa Victoria, hatua ambayo inatarajiwa kuongeza ukuaji wa biashara, utalii na maendeleo ya kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mafuru amewahimiza Watanzania na nchi jirani, kuitumia meli hiyo kama fursa ya kuendeleza biashara na utalii, akibainisha kuwa Ziwa Victoria ni ziwa kubwa zaidi barani Afrika lenye uwezo mkubwa wa kusafirisha mizigo, abiria na kuvutia watalii.
Katika sekta ya utalii, amesema kwa sasa wanapokea watalii kutoka nchini Kenya takribani 240,000 na Uganda zaidi ya 6,000, ambao wengi hutumia usafiri wa anga na barabara.
Hivyo, uzinduzi wa MV New Mwanza umefungua ukurasa mpya kwa kuonesha kuwa watalii sasa wanaweza kuzunguka ukanda wa Afrika Mashariki kwa kutumia usafiri wa majini ulio rahisi, salama na nafuu.
“Leo hii Serikali imeithibitishia dunia kuwa usafiri wa majini ni muhimu wa kukuza utalii na biashara ndani ya Afrika Mashariki,” amesema Mafuru.
Uzinduzi wa MV New Mwanza unatajwa kuwa hatua muhimu katika kutangaza Tanzania kama kitovu cha usafiri, biashara na utalii katika ukanda wa Maziwa Makuu na Afrika kwa ujumla.



