Mwakibete: Hakuna hasara ujenzi wa reli Tabora – Kigoma

SERIKALI imefafanua kuwa hakuna hasara yoyote iliyosababishwa na ununuzi wa mkandarasi wa ujenzi wa njia ya reli ya Tabora-Kigoma, kwa kuwa ulifuata taratibu zote za manunuzi ikiwemo majadiliano kwa lengo la kuhakikisha gharama sahihi za mradi zinapatikana.

Hayo yalielezwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Fred Mwakibete wakati akijibu swali la nyongeza na msingi la mbunge wa Kisesa Luhaga Mpina.

Katika maswali yake, Mpina alitaka kujua kwa nini serikali ilitumia njia ya single source kumpata Mkandarasi CCECC wa Mradi wa SGR LOT 6 Tabora-Kigoma na kusababisha hasara ya trilioni mbili.

Akijibu swali hilo, Mwakibete anasema Sheria ya Manunuzi ya Umma imeainisha njia mbalimbali za manunuzi ya mkandarasi zinazoweza kutumiwa na serikali ikiwa ni pamoja na njia ya Single Source.

Aidha, anasema Manunuzi ya Mkandarasi kwa kipande cha Tabora-Kigoma yalifuata Sheria za Manunuzi ambayo ni Sheria ya Manunuzi ya Umma Namba 7 ya Mwaka 2011 na kanuni zake Na. 161 (1) (a)-(c) ya Kanuni za Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2013 na Marekebisho yake (Mwaka 2016).

“Mheshimiwa Spika, naomba kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako tukufu kuwa hakuna hasara yoyote iliyosababishwa na ununuzi wa mkandarasi kwa kuwa alifuata taratibu zote za manunuzi,” alieleza Naibi Waziri huyo

Hata hivyo, anasema makadirio ya gharama za kihandisi yalikuwa Dola za Marekani bilioni 3.066 sawa na Sh trilioni 7.2 ikilinganishwa na gharama halisi za bei ya Mkandarasi baada ya majadiliano ambayo ni Dola za Marekani bilioni 2.216 sawa na Sh trilioni 5.2.

“Hii ni baada ya majadiliano yaliyosababisha kuokoa Dola za Marekani milioni 273.9 sawa na Sh bilioni 632.74 kutoka kwenye zabuni ya awali ya Dola za Marekani 2.4 sawa na Sh trilioni 5.8,” alisisitiza.

 

Habari Zifananazo

Back to top button