Mwalimu auawa kwenye bajaji Chato

GEITA: MWALIMU wa Shule ya Sekondari ya Magufuli wilayani Chato mkoani Geita, Cathbert Julius ,42, amevamiwa na kuuwawa kikatili akiwa kwenye bajaji aliyokuwa akitumia kusafirisha nguruwe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Safia Jongo limethibitisha kutokea tukio hilo katika taarifa yake kwa waandishi wa habari Julai 08, 2025.

Taarifa imesema mara ya mwisho Julai 05, 2025 majira ya saa 2 usiku mwalimu Cathbert alionekana eneo la Mkongolo karibu na Kidongo Chekundu akiwa na bajaji aina ya Sinoray yenye namba MC.337DLG.

Imeelezwa kuwa ndani ya bajaji hiyo alikuwa amebeba nguruwe wanne aliokuwa akiwapeleka Geita mjini na bajaji hiyo ilipata hitirafu na ndipo alivamiwa na kundi la waharifu waliomjeruhi vibaya.

“Julai 6, 2025 majira ya saa 5 asubuhi, mwili wake ulipatikana kando ya barabara ya lami eneo la Kidongo Chekundu ukiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake”, taarifa imesema.

Taarifa imethibitisha kuwa tayari linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo inagwa bajaji pamoja na nguruwe waliokuwa wakisafirishwa tayari wamepatikana.

“Watuhumiwa hao ni Nyarukamo Mugasa (42), mfanyabiashara, Aron Elias (35) mkulima, Octavius Silvery (25) dereva bajaji na Bukeye Joseph ( 17) utingo wa bajaji wote kutoka Manispaa ya Geita”, imeelezwa.

Jeshi la Polisi limesema kuwa linaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo ambapo watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi wa tukio kukamilika.

Aidha, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi wote kushirikiana kwa karibu na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa sahihi kwa wakati kuhusu vitendo vya kiharifu na watu wote wenye mienendo ya uharifu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button