Mwamposa, maaskofu waungana kuombea taifa, Rais

MTUME wa Kanisa la Inuka na Uangaze, Boniface Mwamposa pamoja na maaskofu wengine zaidi ya wanne wameongoza ibada maalumu ya kuliombea taifa na kumuombea Rais Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi mwema wenye mafanikio kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Mtume Mwamposa aliongoza ibada hiyo wakati wa uzinduzi wa jengo jipya ‘hema’ la kanisa hilo uliofanyika Kawe katika viwanja vya Tanganyika Pakers mkoani Dar es Salaam jana.
Akizunguumza mara baada ya uzinduzi huo uliofanywa na Rais Samia, Mtume Mwamposa alisema ujenzi wa hema hilo yalikuwa ni maono yake ya muda mrefu na kukamilika kwake kunafungua milango ya kiuchumi, kiroho, baraka na mafanikio kwa waumini wake.
Alisema uwepo wa Rais Samia katika tukio hilo ni jambo la kipekee na lenye kuonesha jinsi viongozi wa kitaifa wanathamini mchango wa taasisi za dini katika kujenga maadili na mshikamano wa jamii.
“Ni baraka sana na ni furaha Rais kuwepo hapa kwa sababu yeye ndiye anayesimamia serikali uwepo wake hapa tutamuombea na wananchi wanajua kuwa Rais wetu yupo pamoja nasi,” alisema.
Akitoa historia fupi Askofu wa Kanisa hilo, Mpeli Mwaisumbe alisema awamu ya kwanza ya ujenzi wa hema hilo ulianza Juni 2024 na kukamilika Julai 2025.
Alisema ujenzi huo umehusisha mahema manne yaliyojengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa meta za mraba 28,000 na kila hema moja lina ukubwa wa meta 25 kwa 200 na kufanya jumla kuwa meta 100 kwa 200.
Kwa awamu ya pili ya ujenzi huo utahusisha mahema mawili yenye ukubwa wa meta 40 kwa 200 na utakapo kamilika ujenzi huo utagharimu Sh bilioni 15 zilizotokana na sadaka na miradi mingine.
Kukamilika kwa ujenzi wa mahema hayo kunafanya kanisa hilo kuwa na uwezo wa kubeba waumini 50,000 kwa wakati mmoja.
Alisema kwa zaidi ya miaka nane kanisa hilo limekuwa likitoa huduma za kiroho kwa jamii kutokea Kawe na limefanikiwa kuwasaidia wananchi kiroho, kijamii na kiimani.
Aidha, Askofu Mwaisumbe aliiomba serikali kuwaruhusu watumie eneo hilo kuabudu na liwe la kudumu akisema uwepo wa Rais Samia katika uzinduzi huo unathibitisha kuwa kiongozi huyo anathamini uhuru wa kuabudu.
Naye baba Askofu David Mwasota alisema uzinduzi wa hema hilo unatoa ishara kuwa serikali na kanisa ni washirika muhimu wa maendeleo ya mwili na kiroho na kuzitaka taasisi hizo kuendelea kushirikiana na serikali ili kujenga taifa lenye haki, amani na hofu ya Mungu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) mkoa wa Dar es Salaam, Shehe Mohamed Mawinda aliwataka Watanzania kudumisha amani kwa kuangalia mfano wa hali za nchi jirani zinazoizunguka Tanzania kwa sasa.
Alisema Rais ameonesha mfano kwa kushirikiana na taasisi za kidini ili kudumisha amani na mshikamano