Mwanafunzi afariki dunia stendi akisubiri basi

MOROGORO: MWANAFUNZI wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Jordan kilichopo mkoani Morogoro Magnos Mkinga ,22, amefariki dunia ghafla wakati akusubiria gari stendi kuu ya mabasi ya Msamvu.
Inadaiwa kuwa alizidiwa na homa wakati akisubiri usafiri wa kuelekea Ruvuma kwa ajili ya matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumapili, Machi 2, 2025, na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, imeeleza “Mtu aliyefahamika kwa jina la Magnos Simon Timoth Mkinga ,22, mwanachuo wa Chuo Kikuu cha Jordan, mwaka wa kwanza, mkazi wa Kipera, mkoani Morogoro alizidiwa ghafla na kujilaza chini mbele ya dada yake aitwaye Anna Osward Mbonde ,42, mkazi wa Kibaha wakati wanasubiri usafiri wa basi la Kampuni ya Super Feo kwenda Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma kwa ajili ya matibabu.”
Juhudi za kumuokoa ziliendeshwa haraka kwa msaada wa gari la polisi iliyokuwa doria eneo hilo. Hata hivyo alipofikishwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro madaktari walithibitisha kuwa alishafariki dunia.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu alikuwa na historia ya matatizo ya kiafya na kwamba familia yake ilikuwa katika harakati za kumpeleka kwenye matibabu maalum ili kuboresha afya yake.
Viongozi wa usalama wamewataka wananchi kuwa makini na afya zao na kutafuta msaada wa haraka pale mtu anapoonyesha dalili za kuzidiwa ghafla.
Kifo cha Magnos kimeacha simanzi kubwa kwa familia yake, ndugu, marafiki na wanafunzi wenzake wa Chuo Kikuu cha Jordan. Wengi wameeleza masikitiko yao na kutuma salamu za pole kwa familia ya marehemu..



