Mwanaharakati Algeria ahukumiwa miaka 10 jela

MAHAKAMA ya Constantine nchini Algeria imemhukumu mwanaharakati wa upinzani wa Franco-Algeria, Amira Bouraoui kifungo cha miaka 10 jela bila kuwepo mahakamani na miezi sita kwa mwandishi wa habari anayetuhumiwa kumsaidia kutorokea Ufaransa.
Bouraoui alishtakiwa kwa kuondoka katika eneo hilo kinyume cha sheria baada ya kuvuka mpaka kati ya Algeria na Tunisia Februari 3, mwaka huu na kukaidi marufuku ya kutoka, kabla ya kukamatwa Tunisia alipokuwa akijaribu kupanda ndege kuelekea Paris Ufaransa.
Mwanaharakati huyo alienda Ufaransa siku tatu baadaye, licha ya jaribio la mamlaka Tunisia kumrejesha Algeria.
Bouraoui alipata umaarufu mwaka 2014 kwa kuhusika kwake katika vuguvugu la Barakat dhidi ya muhula wa nne wa Rais Abdelaziz Bouteflika, kabla ya kujihusisha na vuguvugu la maandamano ya Hirak Rif na kufanya kazi katika kituo cha redio M cha upinzani.