Mwanaisha Mndeme atwaa fomu kugombea ubunge

WAZIRI wa Kivuli wa Viwanda na Biashara, kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Wakili Mwanaisha Mndeme amechukua fomu ya kuwania ubunge kupitia chama hicho kwenye jimbo la Kigamboni jijini Dar es Salaam Uchaguzi Mkuu 2025.
Akizungumza leo mara baada ya kuchukua fomu,Wakili Mndeme amewaambia waandishi wa habari kuwa pindi akipata ridhaa ya kuwa Mbunge wa Kigamboni atakwenda kutatua changamoto zinazowakumba wananchi wake na kufanya kuwa sauti ya Kigamboni.
Aidha,Wakili Mndeme amesema kwa kipindi kirefu wananchi wakigamboni wamekuwa na changamoto ya miundombinu.
“Leo hii kigamboni kuna changamoto kubwa ya miundombinu kwa mfano kata ya PembaMnazi, Kata ya Kisarwe 2 hakuna kabisa barabara,wananchi wanalazimika kutumia hela nyingi kusafiri, nikipata nafasi ya ubunge nitahakikisha naziondoa hizi changamoto,” amesema amehaidi wakili huyo.
Amesema pindi akipata ridhaa ya Mbunge wa Kigamboni atapigani sera ya uhifadhi kwa wavuvi ili waweza kunufaika na mifuko ya uhifadhi ya jamii ikiwemo kupata mafao .
“Nitakuwa sauti ya wavuvi maana kigamboni watu wengi ni wavuvi ili kutatua changamoto zinazowakumba wavuvi ili wavuvi waweze kufanya kazi zao bila kikwazo,”amesema.
Kuhusu Sera na sheria,Wakili Mndeme, amesema pindi akipata ridhaa ya kuwa mbunge wa Kigamboni atakapokwenda bungeni atatumia taaluma yake ya sheria kuhakikisha zinatungwa sheria zitakazoweza kulinda maslahi mapana ya rasilimari za nchi.
Akizungumzia kuhusu chama chake kushiriki uchaguzi,Wakili Mndeme amesema chama chake kimeshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu ili kutimiza haki ya mpiga kura huku akiwahimiza wananchi kujitokeza kwenye kupiga kura.



