MWANZA: MWANAMKE mmoja ambaye jina lake bado halijafahamika amekutwa amefariki dunia katika nyumba ya kulala wageni (Guest House) iliyopo wilayani Misungwi, mkoani Mwanza.
Kwa mujibu wa taarifa za Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, tukio hilo lilitokea katika nyumba ya kulala wageni iitwayo First and Last Guest House, ambapo marehemu alikutwa ndani ya chumba namba tatu akiwa amefariki dunia.
Uchunguzi wa awali wa polisi umebaini kuwa mnamo tarehe 18 Machi 2025, majira ya saa 1 jioni mgeni mmoja aliyejiandikisha kwa jina la Bilal William, mkazi wa Geita, alifika katika nyumba hiyo ya kulala wageni akitokea Chato kuelekea Nzega. Bilal alipokelewa, akapewa chumba namba tatu, na kuweka mizigo yake.
Baadaye, majira ya saa 4 usiku, Bilal alionekana akitoka chumbani kwa madai ya kwenda kutafuta chakula. Hata hivyo, ilipofika usiku mkubwa, alirudi akiwa ameongozana na mwanamke ambaye sasa ndiye aliyekutwa amefariki dunia.
Inadaiwa kuwa mnamo saa 12 asubuhi wahudumu wa nyumba hiyo walipokuwa wakifanya usafi, waligundua kuwa mlango wa chumba hicho ulikuwa umefungwa kwa nje, jambo lililowatia mashaka. Walipoamua kuufungua na kuingia ndani, walimkuta mwanamke huyo akiwa amefungwa kanga usoni, na mwili wake ukiwa na mikwaruzo huku akiwa uchi. Mwanaume aliyekuwa naye hakuonekana mahali hapo.
Mwili wa marehemu umepelekwa hospitali ya Wilaya ya Misungwi kwa uchunguzi na utambuzi. Mpaka sasa, bado hajafahamika rasmi. Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu tukio hili.