BUTIAMA, Mara: MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Hamza Johari ameshiriki mazishi ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Mstaafu Frederick Werema, yaliyofanyika leo Januari 04, katika Kijiji cha Kongoto, Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara.
Akizungumza wakati wa utoaji wa salamu za pole, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amesema kuwa Jaji Werema alijitolea kwa hali na mali katika kuhakikisha kwamba serikali inatekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria na kwa uwazi.
Alipambana na changamoto nyingi zilizokuwa zikiikabili tasnia ya sheria na hakusita kuanzisha mabadiliko yaliyoleta matokeo chanya kwa wananchi na taifa kwa ujumla. Huu ni urithi mkubwa ambao utaendelea kuwa mfano na msingi wa kazi yetu sote tunaoendelea nayo leo.
SOMA: Jaji Werema alishiriki mabadiliko ya Vyama Vingi 1993
Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesisitiza kuienzi na kuiendeleza misingi na mifumo ya sheria aliyoianzisha Jaji Werema kwa ustawi wa sekta ya sheria na taifa kwa ujumla.
“Kazi yake ni nguzo ya msingi kwa maendeleo ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kwa maendeleo ya sekta ya sheria nchini kwa ujumla,” amesema Johari.
Johari amesema marehemu Jaji Werema, ameacha alama isiyofutika katika tasnia ya sheria na Utumishi wa Umma nchini, atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa kwa taifa katika masuala mbalimbali ya kisheria na utendaji wa haki.
Jaji, Frederick Mwita Werema amefariki Desemba 30, 2024 akiwa kwenye matibabu Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuagwa kiserikali Januari 02, 2025 Ukumbi wa Karimjee.
Jaji Werema amezaliwa Oktoba 10, 1955 atakumbukwa kwa uzalendo wake na utetezi wa haki, huku akihudumu nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali tangu 2009 hadi 2014 alipojiuzulu.
SOMA: Kwaheri Jaji Werema