WAKATI Kada ya Sheria ikiondokewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Frederick Mwita Werema aliyefariki Desemba 30, 2024 katika matibabu kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, taifa pia linaomboleza kifo chake.
Jaji Werema aliyezaliwa Oktoba 10, 1955 atakumbukwa kwa uzalendo wake na utetezi wa haki.
Amekuwa pia mshirika mzuri wa masuala ya kijamii, akiondoka duniani kama Mwenyekiti wa Parokia ya Mtakatifu Martha, Mikocheni Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
Viongozi mbalimbali wameendelea kumiminika kwenye Ukumbi wa Karimjee kwa ajili ya kumuaga kiongozi huyu huku Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitarajiwa kuongoza shughuli hiyo ya kiserikali.
Aidha viongozi mbalimbali wameendelea kutuma salamu za pole, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ametoa pole kwa familia, Jaji Mkuu, Mwanasheria Mkuu, ndugu, jamaa na marafiki wa Jaji Werema.
Jaji Werema, anatarajiwa kuzikwa Butiama mkoani Mara Januari 04.