GEITA; WALIMU wakuu shule za msingi ndani ya Halmashauri ya Mji wa Geita wamekutana kutafuta suluhu la mwandiko mbaya kwa watoto, ambapo inatajwa kuwa kiini cha matokeo mabaya kwa shule za umma.
Walimu hao wamekutana katika shule binafsi ya WAJA iliyopo mjini Geita, ambayo inatajwa kama kinara wa mwandiko bora ili kubadilishana uzoefu na kuwasaidia wanafunzi wa shule za umma.
Ofisa Taaluma Halmashauri ya Mji wa Geita, Khadija Ubuguyu amethibitisha hayo katika kikao kazi cha kubadilishana uzoefu kilichofanyika katika Shule ya Msingi ya WAJA iliyopo mjini Geita.
Khadija amesema wamechanguza na kubaini mwandiko ni tatizo ndani ya halmashauri hiyo na hivyo kuamua kushirikiana na shule ya WAJA, ambayo imekuwa kinara katika suala la uandishi wa insha kitaifa.
Amesema wameamua kulibeba suala la mwandiko kwa uzito wake, kwani muundo wa mitihani ya taifa kwa sasa imebadilika kutoka kuwekea alama jibu sahihi na sasa watoto wanatakiwa kujibu kwa kuandika.
“Sasa hivi muundo umebadilika watoto wanatakiwa waandike kwa mikono yao, sasa kwa utafiti wetu mdogo tuliofanya tumegundua kwamba hali siyo nzuri kwenye miandiko ya watoto.
“Tumegundua kwamba WAJA wapo wataalamu wa herufu, WAJA wao wana mwandiko wa aina moja, nasi tumeona kumbe inawezekana pia kuwa na mwandiko wa aina moja kwa halmashauri nzima,” amesema.
Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Kivukoni, Ndatu Maduka amesema walimu wakuu wa shule za msingi halmashauri ya mji wa Geita wameitazama shule ya WAJA kama eneo sahihi kwa wao kupata mbinu sahihi ya kufundisha watoto mwandiko mizuri.
“Tumechunguza tumeona shule za WAJA wameandika miandiko mizuri, inasomeka na mwalimu mkuu wa hapa amekubali kuja kutupa ujuzi wa kubadilishana naye uzoefu,” amesema.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kalangalala, Regina Cosmas amekiri wazi kwamba endapo suala la miandiko ya watoto halitatazamwa kwa ukubwa wake basi litakachangia watoto kufeli.
“Kama mwanafunzi hakuandika vizuri maana yake anaweza akakosa swali licha ya kuwa analifahamu, lakini akalikosa kutokana na mwandiko mbaya,” amesema.
Mkurugenzi wa Shule za WAJA, Chacha Wambura ameahidi kuwapa ushirikiano walimu wakuu Shule za Halmshauri ya Mji Geita, ambapo amewahakikishia ushirikiano ili kuzima tatizo la mwandiko mbaya.
Amesema ni wazi kwamba shule yake imewekeza nguvu kwenye mwandiko mzuri, kwani mwandiko mbaya haumshawishi msahihishaji kusoma majibu ya mwanafunzi alichokiandika.