Mwandishi HabariLEO atwaa tuzo mabadiliko tabianchi

DAR ES SALAAM; MWANDISHI wa gazeti la HabariLEO na Dailynews Digital, Aveline Kitomary ameibuka mshindi wa kwanza katika Tuzo ya Mwandishi Bora wa Habari za Mabadiliko ya Tabianchi zijulikanazo kama Media4climate Competition 2024.

Tuzo hizo zimetolewa na shirika lisilo la kiserikali la YSO Tanzania, linalojihusisha kuwajengea uwezo vijana kuhusu masuala ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi, nishati na masuala ya jinsi.

Aveline alikabidhiwa tuzo hiyo na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Job Runhaar leo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa utoaji tuzo hiyo na mafunzo kwa vijana Balozi Runhaar amesema mabadiliko ya tabianchi kwa sasa ni kitu ambacho kinazungumzwa na dunia nzima kutokana na athari kwa zake kwa jamii.

“Ni jukumu la vijana kusimama sasa hasa wanahabari kutoa elimu kwa jamii namna bora ya kuzuia na kukabiliana na athari ambazo tayari zimeshajitokeza,”amesema .

Kwa upande wake Aveline  amesema kwa kipindi cha mwaka 2023 ameandika habari na makala nyingi za mabadiliko ya tabianchi, akiangazia upande wa afya, jinsia,mazingira na namna bora ya kukabiliana na mabadiliko hayo.

“Ninamshukuru Mungu kwa kupata tuzo hii, kwa kipindi cha mwaka jana niliripoti mkutano wa mabadiliko ya tabianchi COP28 uliofanyika Dubai Falme za Kiarabu, hivyo nafurahi kutambua mchango wangu katika hili na pia nawashukuru wasimamizi wangu na mabosi wangu kwa kunipa ushirikiano mkubwa wakati wote,”amesema Aveline.

Habari Zifananazo

Back to top button