Mwandishi TSN ashinda tuzo TMA

MWANDISHI wa habari mwandamizi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) Zaituni Mkwama, ameshinda tuzo ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) akiwa mwandishi bora wa taarifa za mamlaka hiyo.

Tuzo hizo zimetolewa jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka hiyo, Jaji Mshibe Ali Bakari.

Advertisement

Akizungumza katika ugawaji wa tuzo hizo, Jaji Bakari amewataka waandishi wa habari kuandika habari za hali ya hewa kwa kuwa ni za uhakika, kwani serikali imewekeza mitambo bora na ya uhakika.

“Hivi sasa hatutegemei mlio wa ndege wala ishara za mnyama kuhusu kujua hali ya hewa, ipo mitambo ya uhakika inayojiongoza yenyewe katika kutambua hali ya hewa,” amesema.

SOMA: TMA yakabidhiwa rada mbili

Jaji Mshibe ameeleza kuwa waandishi ni nguzo muhimu katika kutetea taifa kwa namna yoyote ile akieleza kuwa kinyume chake ni kusababisha maafa.

Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk.Ladislaus Chang’a, Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri Dk. Hamza Kabelwa amesema wamekuwa wakitoa mafunzo kwa waandishi ndani na nje ya nchi ili kuwajengea uwezo katika kuhakikisha wanaandika habari zenye weledi.

Tuzo hizo zimetolewa kwa waandishi wa habari wa magazetini, elektroniki na habari za mtandaoni.