Mweli: Matumizi ya mbolea yafikia tani laki nane nchini

DODOMA: MAMLAKA ya udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imeongeza tija ya matumizi ya mbolea kwa wakulima nchini hadi kufikia tani 800,000.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli wakati akizindua Kongamano la Kwanza la Mbolea Oktoba 11-12, katika Ukumbi wa Mikutano wa JK Nyerere, uliopo Wizara ya Fedha, jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli wakati akifungua Kongamano la Kwanza la Mbolea linalofanyika Oktoba 11 na 12, 2024 katika Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.

“Tumeongeza matumizi ya mbolea mpaka tani laki 800,000 kwa mwaka 2024 kutoka tani 360,000 mwaka 2021/2022 kipindi ambacho mpango wa utoaji wa mbolea ya ruzuku ulipoanzishwa na Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan hivyo tunavyoona maendelea haya hatuna budi kumpongeza Mhe. Rais kwa kuendelea kutoa ruzuku kwa wakulima ili wazalishe kwa tija,” amesema Mweli.

Advertisement

Katibu Mkuu amezipongeza kampuni za ndani zinazozalisha mbolea kuendelea kuzalisha mbolea kwa wingi na ametoa rai kwa wawekezaji mbalimbali kuja kuzalisha mbolea nchini na kuhakikisha matumizi ya mbolea yana akisi na afya ya udongo ili Tanzania ifikie malengo ya kuwa kitovu cha uzalishaji na usambazaji wa mbolea katika mataifa mengine barani Afrika.

Kongamano hilo limehudhuriwa pia na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara Kilimo, Mifugo na Uvuvi wakiwemo wadau wa maendeleo pamoja na wawakilishi kutoka mataifa mbalimbali.

Kongamano hilo ni la siku mbili ambapo washiriki watajadili masuala mbalimbali ya uendelezaji wa tasnia ya mbolea nchini, chini ya kauli mbiu “Kilimo ni Mbolea”.

SOMA: Ruzuku ya mbolea kuigharimu serikali Sh bilioni 300