Mwenge wa Uhuru wazindua madarasa 14 sekondari Kagongwa
MWENGE wa Uhuru umezindua vyumba 14 vya madarasa vilivyojengwa kwa thamani zaidi ya sh millioni 470 katika shule ya sekondari Kagongwa iliyopo Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga.
Uzinduzi huo umefanyika leo baada ya kiongozi wa mbio hizo kitaifa, Abdalla Kaim kujiridhisha na ujenzi wa vyumba hivyo ulioendana na thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali Kuu, nguvu za wananchi na mapato ya ndani ya halmashauri.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Alloyce Nyanda amesema shule ilianza kujengewa mwaka 2021 ambapo ina kidato cha kwanza hadi cha nne baada ya majengo kukamilika.
“Vyumba vya Madarasa 14 vimejengwa ambapo vyumba sita vilijengwa kwa nguvu za wananchi kwa Sh millioni 15 mpaka usawa wa renta na halmashauri ikakamilisha kwa mapato ya ndani zaidi ya Sh milioni 100 na fedha za Serikali Kuu zimetimika Sh milioni 470 kujenga vyumba vya madarasa nane.” amesema Nyanda.
Mwalimu Nyanda amesema katika fedha zilizotolewa na Serikali Kuu zimeweza pia kujenga maabara tatu, maktaba moja,matundu ya vyoo mawili na jengo la utawala.
Diwani wa kata ya Kagongwa Ismail Masolwa alisema kuna wanafunzi kidato cha kwanza na pili wanafunzi zaidi ya 2000 bado kuna msongamano aliomba serikali kuwashika mkono tena ili kuongeza vyumba vingine vya madarasa ili mwakani watoto wasikose nafasi.
Kaim amesema miradi mingi wameikagua mkoani Shinyanga imeonekana yote imekidhi viwango hivyo kasoro ndogondogo zilizojitokeza zirekebishwe vizuri na watoto waendelee kupata elimu wakiwa kwenye mazingira bora.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mboni Mhita baada ya kuupokea mwenge huo amesema utazindua,kuona na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi 17 yenye thamani ya Sh bilioni 5.2 na kukimbizwa umbali wa kilomita 258.1.